Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ndg. Gerson Msigwa, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tamasha la utamaduni, Agosti 23, 2026, katika Kambi ya Wapigania Uhuru Mazimbu, mkoani Morogoro.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Tamasha la Nne la Kitaifa la Utamaduni linalotarajiwa kufanyika mkoani Morogoro kuanzia Agosti 25 hadi 29, 2026, limeelezwa kuwa nyenzo ya kufungamanisha uchumi na kuendeleza urithi wa Watanzania kwani linalenga kuendeleza, kuhifadhi na kutangaza urithi wa Tanzania pamoja na kuimarisha utambulisho wa Taifa na historia yake kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa ameyasema hayo Agosti 23, 2026 wakati akitoa taarifa ya Serikali mbele ya Waandishi wa Habari katika Kambi ya Wapigania Uhuru iliyopo Mazimbu mkoani Morogoro.

Bw. Msigwa ameeleza kuwa, kufanyika kwa tamasha hilo kila mwaka, ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kulinda, kuendeleza na kutumia utamaduni wa Mtanzania kama nyenzo ya kujenga maadili, kuimarisha utaifa na mshikamano, kukuza uchumi bunifu na kukuza fursa za ajira na biashara pamoja na kuitangaza Tanzania kupitia utalii wa kiutamaduni.

“Tamasha la Utamaduni limeandaliwa kwa mtazamo mpana unaounganisha utamaduni na uchumi kwa lengo la kuhakikisha sanaa na urithi wa Taifa vinakuwa sehemu ya kuchochea maendeleo na kuongeza fursa za kiuchumi kwa wananchi. Tamasha hilo siyo la kuangalia tu bali kushiriki, kujifunza, kubuni, kufanya biashara na kujenga uhusiano”, amesema Bw. Msigwa.

Akifafanua kuhusu kauli mbiu ya tamasha hilo ambayo ni; Utamaduni Wetu, Nguzo ya Maadili, Uchumi Jumuishi na Utaifa, Karibu AFCON 2027, amesema inasisitiza maadili, uchumi jumuishi na Utaifa. Vile vile, inahusisha maandalizi ya Tanzania kwa kushirikiana na Kenya na Uganda kuwa wenyeji wa AFCON. 

Ameongeza kuwa, tamasha hilo linatarajiwa kuikutanisha mikoa 26, vikundi vya utamaduni 28, Wasanii 30, wajasiriamali 70, vijana takriban 5,000, taasisi za washirika 70 pamoja na wananchi na wageni wanaokadiriwa kufikia 150,000.

Aidha, linatarajiwa kuwa na shughuli 120 ikiwemo maonesho ya vyakula vya asili 100, bidhaa za utamaduni na ubunifu zaidi ya 150 pamoja na fursa za biashara zinazokadiriwa kufikia 70.