NA FAUZIA MUSSA

Kampuni ya Mwani Zanzibar ZASCO na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) zimesaini makubaliano ya ushirikiano yenye lengo la kuhakikisha uzalishaji wa mbolea inayotokana na mwani unakidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Makubaliano hayo yalisainiwa, wakati wa Kongamano la Uchumi wa Buluu lililofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Kwanza ikiwa ni sehemu ya tamasha la Kizimkazi 2026.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mkurugenzi Mkuu wa ZASCO Dk. Masoud Rashid Mohammed amesema Serikali kupitia Wizara YA Uchumi wa Buluu na Uvuvi inaendelea na ujenzi wa kiwanda cha kuchakata mwani kinachotarajiwa kuanza kufanya kazi ya uzalishaji siku za karibuni baada ya kuzinduliwa.

“kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha mbolea inayotokana na mwani, mara baada ya kuzinduliwa rasmi” . Alisema Dk. Massoud 

Alifahamisha kuwa kupitia makubaliano hayo, TFRA na ZASCO watashirikiana kufanya majaribio na tathmini ya ubora wa mbolea hiyo kabla ya kuanza kutumika ili kuhakikisha mbolea itakayozalishwa inafikia viwango vinavyotakiwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA Joel Laurent alieleza kuwa taasisi hiyo ina jukumu la kudhibiti mnyororo wa thamani wa mbolea hivyo itahakikisha bidhaa hiyo inapitia hatua zote muhimu za uhakiki, upimaji na usajili kwa mujibu wa taratibu na viwango vilivyowekwa.

“Tumeshaingia makubaliano tutahakikisha tunakuza sekta ya mbolea na nakuza sekta ya kilimo kwa ujumla tukitarajia kupata tija kupitia matumizi sahihi ya pembejeo kama mbolea, hii inayotokana na mwani” alisema

Alieleza kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuunganisha sekta ya Uchumi wa Buluu na kilimo, hususan katika kuongeza thamani ya mwani na kuzalisha bidhaa zitakazoweza kuwasaidia wakulima kuongeza tija.

Makubaliano hayo yameelezwa kuwa ni hatua nzuri kuelekea mapinduzi ya Uchumi wa Buluu, huku yakilenga kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za Serikali, kuongeza thamani ya rasilimali za baharini na kuchangia maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.