NA FAUZIA MUSSA
NAIBU Waziri Mkuu Mstaafu, Dk. Doto Mashaka Biteko, amesema mbio za ngalawa zina nafasi kubwa katika kutumia bahari kama uwanja wa kuendeleza michezo, utamaduni na shughuli za kiuchumi, ikiwemo uchumi wa buluu na utalii.
Dk. Biteko aliyasema hayo katika hafla ya mashindano ya mbio za ngalawa yaliyofanyika katika pwani ya Kizimkazi mkunguni Mkoa wa Kusini Unguja, ikiwa ni sehemu ya Tamasha la Kizimkazi 2026.
Alisema matumizi ya bahari kwa shughuli za michezo na burudani yanaonesha namna rasilimali za bahari zinavyoweza kutumika katika kuendeleza shughuli mbalimbali zenye manufaa kwa jamii.
Alisema mbio hizo pia zinaendelea kuwa sehemu ya urithi wa kiutamaduni wa jamii za pwani na zinapaswa kuendelezwa ili kizazi cha sasa na kijacho kiweze kufaidika na urithi huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Mbio za Ngalawa alisema mashindano hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha, kuunganisha na kuendeleza undugu na mshikamano miongoni mwa wananchi.
Alisema mbio hizo ni urithi wa kiutamaduni ambao umeendelea kudumishwa katika Mkoa wa Kusini Unguja, hivyo mashindano hayo yanapaswa kuendelezwa na kupewa nafasi zaidi.
Mashindano hayo yalishirikisha wananchi kutoka makundi mbalimbali, huku watu wenye ulemavu nao wakishiriki katika shughuli hizo, hatua iliyotoa fursa ya kuonesha kuwa michezo na shughuli za kijamii zinaweza kuwahusisha wananchi bila kujali hali zao.
Baadhi ya wananchi waliohudhuria mashindano hayo walisema mbio za ngalawa zimekuwa kivutio kwa jamii kutokana na kuchanganya michezo, utamaduni na burudani, huku zikitoa fursa kwa wananchi kukutana na kushirikiana.
Walisema kuendelea kwa mashindano hayo Kizimkazi kunaweza kusaidia kuongeza hamasa kwa vijana kushiriki katika michezo na pia kutangaza utamaduni wa Zanzibar kwa wageni wanaofika katika eneo hilo.
Wananchi hao pia walipongeza ushiriki wa watu wenye ulemavu katika mashindano hayo, wakisema hatua hiyo inaimarisha dhana ya ushirikishwaji na kuwapa nafasi watu wa makundi mbalimbali kushiriki katika shughuli za kijamii na michezo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kusini Unguja, Othman Ali Maulid, alipongeza maandalizi ya Tamasha la Kizimkazi, akisema shughuli hizo zimekuwa zikileta pamoja wananchi na kuimarisha amani, upendo na mshikamano.
Alisema mbio za ngalawa zina mchango katika kuchochea maendeleo ya sekta ya uchumi wa buluu na utalii kutokana na kuunganisha michezo, utamaduni na fursa za kiuchumi.
Alisema kuendelezwa kwa mbio hizo kunaweza kuongeza mvuto wa Kizimkazi na Zanzibar kwa ujumla, huku kukitoa nafasi kwa wananchi kushiriki na kunufaika na shughuli za michezo, utamaduni na utalii.
Mashindano hayo yakikutanisha timu mbili za Mchangamle na Mkunguni, huku kila timu ikiwa na manahodha 10.
Fedha na boti vilikabidhiwa kama zawadi kwa mshindi wa mashindano hayo ikiwa ni sehemu ya kutambua juhudi na uwezo wao katika mashindano hayo.

