NA BALTAZAR MASHAKA, NYAMAGANA 

MWENGE wa Uhuru 2026 umeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa tenki la kuhifadhi maji Buhongwa, jijini Mwanza, mradi unaolenga kuimarisha upatikanaji wa maji safi na salama kwa zaidi ya wananchi 80,000 wa Buhongwa na maeneo jirani.

Tenki hilo lenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 10 za maji, utekelezaji wake umefikia asilimia 85 ambapo mradi huo utakapokamilika utasaidia kuhifadhi na kusambaza maji kutoka chanzo cha Butimba kwenda maeneo ya Buhongwa, Sahwa, Kagera, Gwambiti, Nyahingi, Kanindo na Nyashishi.

Akizungumza baada ya kukagua mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2026, Wazo Mwang’onda, aliipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA), kwa usimamizi wa mradi huo na matumizi sahihi ya fedha za Serikali.

Mwang’onda aliitaka MWAUWASA kuhakikisha inamsimamia mkandarasi akamilishe mradi kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa, ili serikali na wananchi wapate thamani ya fedha iliyowekezwa. 

Aidha, aliwataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu hiyo kwa kuhakikisha inalindwa na kutunzwa ili iweze kutoa huduma endelevu kwa muda mrefu. 

Msimamizi wa Miradi wa MWAUWASA, Mhandisi Nuhu Said, alisema mradi wa Buhongwa ni sehemu ya mpango mkubwa wa ujenzi wa matenki matano yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya lita milioni 31 za maji, ulazaji wa mabomba makuu ya kusafirisha maji yenye urefu wa kilomita 40.5 pamoja na vituo viwili vya kusukuma maji.

 Alisema mradi huo unagharimu sh. bilioni 46.2 bila VAT na unatekelezwa kupitia Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira ya Ziwa Victoria, hivyo mradi wote unatarajiwa kuboresha huduma ya maji kwa takribani wananchi 450,000 wa Jiji la Mwanza na maeneo ya pembezoni utakapokamilika.

 “MWAUWASA itaendelea kuhakikisha uwekezaji huu unaleta matokeo chanya yanayolenga kuboresha upatikanaji na usambazaji wa maji safi na salama kwa wananchi, sambamba na kutimiza adhima ya serikali ya kuimarisha huduma ya maji kwa maendeleo kijamii na manufaa ya wananchi,” alisema Mhandisi Said.