Na Mwandishi Maalum, Namtumbo
WAZIRI wa Katiba na Sheria na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo Mkoani Ruvuma Dkt Juma Homera,ameiagiza Halmashauri ya Wilaya Namtumbo kuwaondoa mara moja wakandarasi wabovu wanaosuasua katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Dkt Homera ametoa agizo hilo jana wakati akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Shule Shikizi ya msingi ya Dkt Juma Homera, iliyopo katika Kijiji cha Mageuzi Kata ya Hanga, wilayani Namtumbo.
“Awali mkandarasi wa awali aliyekuwa akijenga shule hiyo alisimamishwa kutokana na kushindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati”alisema Dkt Homera.
Aidha Dkt Homera ameagiza ujenzi wa shule hiyo ukamilike ifikapo Septemba 11,2026 ili iweze kuanza kupokea wanafunzi huku akiahidi kutoa kiasi cha shilingi milioni 12 kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vya shule hiyo na mafundi waendelee kufanya kazi usiku na mchana.
Waziri Dkt Juma Homera alisema,shule hiyo inajengwa kwa ubora na viwango vya hali ya juu na itakapokamilika itakuwa kivutio kikubwa kwa watoto na jamii kwa ujumla.
Dkt Homera ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Namtumbo,amempongeza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Namtumbo Philemon Magesa na wataalam wake kwa kusimamia vuzuri mradi huo unaotarajiwa kumaliza changamoto ya watoto wanaoishi mbali na eneo hilo kutembea umbali mrefu kufuata masomo shule mama ya Mageuzi.
Aidha Dkt Homera,ametoa muda wa mwezi mmoja hadi tarehe 11 septemba mwaka huu mkandarasi anayejenga shule hiyo kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo ili kutoa fursa kwa watoto waanze kusoma katika shule yao mpya.
“Mkandarasi wa kwanza tulimfukuza kutokana na uzembe na kushindwa kukamilisha ujenzi kwa wakati, sasa natoa mwezi mmoja kwa mkandarasi mpya kuhakikisha anakamilisha ujenzi wa mradi huu haraka,serikali imetoa fedha nyingi ili kujenga shule hiyo kwa lengo la kuwanusuru watoto wanaoishi mbali na eneo la shule mama”alisema Dkt Homera.
Homera,ametoa Sh.milioni 12 ili kujenga vyoo katika shule hiyo uku akiwataka viongozi wa Chama cha Mapinduzi ngazi ya kata na wilaya ya Namtumbo kusimamia kwa karibu ujenzi wa shule hiyo ili iweze kukamilika haraka.
Awali akisoma taarifa ya ujenzi Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mageuzi Frolian Chidudu ameeleza Kuwa, ujenzi unaendelea vizuri ikiwa ni siku ya tatu baada ya baada ya kupatikana Kwa mkandarasi mengine.
Wakazi wa kijiji cha Mageuzi na Mlilayoyo wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma,wamemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia Sh.milioni 144 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya msingi Dkt Juma Homera ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 55.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wamesema, wamefurahishwa na mradi huo kwa kuwa utapunguza msongamano wa watoto katika shule mama ya msingi Mageuzi ambayo kwa sasa imezidiwa na wingi wa wanafunzi.
James Mathayo alisema,kujengwa kwa shule hiyo kutamaliza kabisa usumbufu wa watoto wanaoishi kitongoji cha kibaoni kufuata masomo shule ya msingi Mageuzi.
Alisema, shule mpya ya Dkt Homera itasaidia sana kupunguza ajali za mara kwa mara pindi kwa watoto wao wanapotaka kuvuka kutoka upande mmoja wa barabara kuu ya Songea-Makambako kwenda upande wa pili kufuata masomo.
“Shule hii itasaidia kuwapa usalama na kumaliza ajali na vifo kwa watoto hasa wale wanaojaribu kuvuka barabara kutoka upande mmoja wa kwenda upande mwingine,tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia kwa upendo wake mkubwa”alisema Mathayo.
Mkazi mwingine Paul Nyoni,ameipongeza serikali kwa uamuzi wa kujenga shule hiyo ambayo ikikamilika itapunguza msongamano wa watoto katika shule ya msingi Mageuzi ambayo ina idadi kubwa ya wanafunzi.
“Kwa kweli tunampongeza sana Rais wetu kwa kutuletea fedha hizi zaidi ya Sh.milioni 144 ili kujenga shule hii,watoto wetu walikuwa wanapata shida kutokana na msongamano mkubwa madarasani katika shule ya mama ya Mageuzi”alisema.
Diwani wa kata Sixbert Njewele,ameishukuru serikali kwa kuwajengea watoto wao shule bora na ya viwango na kubainisha kuwa,awali hali ilikuwa tete kutokana na msongamano wa wanafunzi katika shule ya msingi Mageuzi.
Awali Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mageuzi Frolian Chidodo alisema,serikali ilitenga Sh.milioni 144 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya kupitia program ya EP4R tangu mwezi Februari 2026 ili kupunguza wingi wa wanafunzi katika shule ya msingi Mageuzi wapatao 1,245.
Alisema,lengo la Serikali ni kuhakikisha shule moja haizidi wanafunzi 800,hivyo mradi huo wa vyumba sita vya madarasa unalenga kuleta ufanisi wa kimapinduzi ya elimu katika kijiji cha Mgaeuzi kwa kuhakikisha kunakuwa na uwiano nzuri wa idadi ya wanafunzi na miundombinu ya shule.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi kaka mkuu wa shule ya msingi Mageuzi Baraka Nyikata,ameishukuru serikali kuwaletea shule mpya na kuhaidi kusoma kwa bidii ili waweze kutimiza malengo yao.

