Kizimkazi- Zanzibar
Mamlaka ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi imepongezwa kwa kuendelea kuboresha hali ya utoaji mafunzo katika vyuo vyake kote nchini.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Wanu Hafidh Ameir alipotembelea banda la VETA tarehe 12 Agasti, 2026, kwenye Tamsha la Kizimkazi mkoa wa Kusini Unguja, Zanzibar.
Mhe.Wanu amesema, “nawapongeza kwa kuendelea kuboresha hali ya utoaji mafunzo ya ufundi katika vyuo, hali ya uboreshaji mitaala yenye kuendana na mahitaji ya soko la ajira, lakini pia kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali katika jamii yetu, kundi la wanawake na vijana linaendelea kunufaika na mafunzo haya.”
Kwa upande wake Meneja wa VETA Kanda ya Kaskazini, Monica Mbelle amesema VETA inaendelea kutoa mafunzo kwa kuzingatia mahitaji halisi ya soko la ajira, na hivyo kuwawezesha wahitimu wa mafunzo ya ufundi stadi kuajiriwa, kujiajiri na hata kuajiri wengine.
VETA inashiriki katika Tamasha la Kizimkazi lenye kaulimbiu “Kizimkazi kumenoga, Shangwe na Fursa, ambapo ufunguzi rasmi umefanyika tarehe 12 Agasti, 2026 na kilele kinatarajiwa kuwa tarehe 14 Agasti, 2026.
VETA inaendelea kuwaalika wananchi kutemebelea banda lake katika viwanja vya Dimbani ili kupata taarifa za fursa za mafunzo ya ufundi stadi, bidhaa za ubunifu pamoja na huduma za ufundi wa simu za mkononi.

