Na Meleka Kulwa — Fullshangwe Blog, Dodoma

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda , ameitaka Kamati za Ushauri wa Stadi (Training Advisory Committees – TACs) za Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuwa chachu ya kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanaendana na mahitaji halisi ya soko la ajira na uzalishaji nchini.Ameyasema hayo Agosti 13, 2026 jijini Dodoma wakati akizindua rasmi Kamati hizo, akieleza kuwa wajumbe wake wana nafasi muhimu ya kuwa kiungo kati ya VETA, Serikali, waajiri na sekta binafsi katika kuboresha mafunzo ya ufundi stadi nchini.

Amesema mafunzo ya ufundi stadi hayapaswi kuishia katika kumpa mwanafunzi cheti, bali yanapaswa kumwandaa mhitimu kuwa na ujuzi, umahiri, ubunifu, nidhamu ya kazi na uwezo wa kutumia teknolojia ili kufanya kazi, kujiajiri na kuongeza tija katika uzalishaji.

“Msiwe Kamati za mikutano tu; muwe Kamati za matokeo. Tambueni mabadiliko kabla hayajatokea na mshauri VETA kuchukua hatua mapema,” amesema Prof. Mkenda.

Ameongeza kuwa TACs zinapaswa kusaidia VETA kubaini stadi mpya zinazohitajika katika sekta mbalimbali na kushauri kuhusu maboresho ya mitaala, teknolojia na programu za mafunzo, ikiwemo katika sekta za ukarimu, utalii, sanaa, TEHAMA, uzalishaji, ujenzi, nishati na kilimo.

Huku akibainisha Kuwa  jukumu hilo ni muhimu zaidi wakati Tanzania ikiendelea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo inaweka mkazo katika uchumi imara, jumuishi na shindani pamoja na kujenga uwezo wa watu na maendeleo ya jamii.

Amesema Tanzania haiwezi kujenga uchumi wa kisasa bila kuwa na nguvu kazi yenye ujuzi, akisisitiza kuwa viwanda, uchumi wa kidijitali na uzalishaji wa bidhaa na huduma vinahitaji mafundi, wataalamu wa teknolojia na vijana wenye uwezo wa kutumia maarifa na ubunifu.

Aidha, amewataka waajiri kuwa sehemu ya mfumo wa mafunzo kwa kueleza mahitaji yao ya ujuzi, teknolojia, vifaa na viwango vya utendaji ili VETA iweze kuandaa nguvu kazi inayokidhi mahitaji ya maeneo ya kazi.

Pia, Amesema Kuwa  Serikali itaendelea kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za elimu na sekta ya viwanda kupitia Mpango wa Kitaifa wa Ushirikiano kati ya Taasisi za Elimu na Sekta ya Viwanda katika Ukuzaji wa Ujuzi na Uwezeshaji wa Ajira, uliozinduliwa Februari 9, 2026 jijini Dar es Salaam.

Aidha, amebainisha Kuwa , wajumbe wa TACs wanapaswa kuwa mabalozi wa VETA katika sekta wanazotoka kwa kuwaelimisha waajiri kuhusu fursa za kushirikiana na VETA katika uandaaji wa mitaala, mafunzo kwa vitendo, tafiti, teknolojia na maandalizi ya wataalamu wenye ujuzi unaohitajika.

Pia,amewataka wajumbe hao kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu, weledi, ubunifu, uwajibikaji na uzalendo, akisisitiza kuwa Serikali inawategemea katika kuhakikisha TACs zinakuwa daraja kati ya elimu na ajira pamoja na kuwa injini ya ubora, ubunifu na ushindani wa Taifa.

“Kwa pamoja, tuhakikishe kwamba TACs zinakuwa chachu ya mabadiliko, daraja kati ya elimu na ajira, na injini ya ubora, ubunifu na ushindani wa Taifa,” amesema.