Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa maji na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mhandisi Wolta Kirita amefanya ziara ya kukagua mradi wa maji wa Ushetu – Ulowa uliopo Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama na kujionea maendeleo ya mradi huo.
Mkurugenzi Mkuu akiambatana na baadhi ya timu ya menejimenti kutoka RUWASA makao makuu,Meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga,Meneja wa RUWASA Wilaya ya Kahama pamoja na wasimamizi wa mradi walitembelea mradi huo kutoka Kahama kuelekea Kata ya Mlowa.
Akitoa maelezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA Meneja mradi Mhandisi John Msengi amesema hadi sasa mradi unaendelea vizuri na kwa sasa mradi upo katika hatua nzuri kwani mabomba na matanki ya vijiji vyote yamekamilika na kazi kazi iliyobaki ni bomba kuu pekee ili wananchi waweze kupata huduma ya maji.
Kwa upande wa Meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Julieth Payovela amemhakikishia Mkurugenzi Mkuu kuwa mara tu mradi huo kukamilika pamoja na kuhudumia kata ya Mlowa pia utaweza kuhudumia kata nyingine kumi zilizopo njiani kuelekea kata ya Mlowa.
Akihitimisha ziara hiyo Mkurugenzi Mkuu wa RUWASA ameitaka kampuni iliyopewa kazi ya kujenga mradi huo ikamilishe kazi hiyo mapema ili wananchi waweze kupata maji kwani lengo kuu ni kuhakikisha huduma ya maji inapatikana.
*”Mambo ambayo tumekubaliana na Mkandarasi wa mradi ni kuhakikisha huduma ya maji inapatikana mapema na itasaidia kulinda miundombinu, na hii itasaidia kijiji cha jirani wakiona wenzao wanapata maji basi na wao wanakuwa na uhakika wa kupata maji”* Alisisitiza Mhandisi Kirita.
Akiongea kwa niaba ya Wananchi wa Kata ya Ulowa kijiji cha Ulowa namba mbili Bi.Martha Simon Philipo ametoa shukurani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia RUWASA kwa kuwaletea maji katika kijiji chao kwani kabla ya ujio wa mradi huo wananchi walisumbuka sana kupata huduma ya maji.
Mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya ndani inayoitwa SIHOTECH Engineering Company Limited kwa kushirikiana na Mponela Construction and Company Limited, kwa gharama ya Shilingi 37,518,548,032.35, huku kazi zilizofanyika hadi sasa zikihusisha ununuzi na ulazaji wa mabomba ya chuma yenye urefu wa kilomita 38.382 na mabomba ya HDPE yenye urefu wa kilomita 66.866, pamoja na ujenzi wa vituo vya kusukuma maji, matanki na miundombinu ya kusambaza maji kwa wananchi.

