Na Meleka Kulwa — Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, amesema Serikali itayafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa katika Kongamano la Haki za Ardhi za Wanawake, huku akiahidi kuyawasilisha katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa ili kuimarisha ushiriki wa wanawake katika masuala ya ardhi, mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Ameyasema hayo Agosti 13, 2026, jijini Dodoma wakati akifunga kongamano hilo lililofanyika kwa siku mbili, Agosti 12 hadi 13, likiwakutanisha viongozi wa Serikali, wataalamu wa ardhi, wadau wa maendeleo na viongozi wa wanawake.
Huku akibainisha Kuwa kongamano hilo limewezesha wadau kutengeneza mapendekezo yanayolenga kuimarisha utekelezaji wa sheria za ardhi, kuongeza ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi, kuimarisha mipango ya matumizi bora ya ardhi vijijini na kuongeza uwekezaji katika miradi ya wanawake na vijana.
Aidha, amesema mapendekezo hayo yamegusa umuhimu wa kuhakikisha fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zinawafikia wananchi katika ngazi ya jamii, hususan wanawake ambao wana nafasi muhimu katika shughuli za uzalishaji na uhifadhi wa mazingira.
Pia, amesisitiza kuwa haki za wanawake katika umiliki wa ardhi zinahitaji ushiriki wa jamii nzima, akiwataka wanaume kuongeza ushiriki wao katika mijadala na juhudi za kuhakikisha wanawake wanapata nafasi katika kufanya maamuzi yanayohusu ardhi na maendeleo.
Aidha, amebainisha umuhimu wa wanawake kushiriki katika majukwaa ya kimataifa yanayohusu ardhi, mazingira na mabadiliko ya tabianchi, ili kuhakikisha changamoto na mitazamo yao inazingatiwa katika maamuzi yanayofanyika katika ngazi ya kimataifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Landesa, Godfrey Mase, amesema Kampeni ya “Linda Ardhi ya Mwanamke” ilizinduliwa Tanzania mwaka 2019 ikiwa na wajumbe 25 na imeendelea kukua hadi kufikia wajumbe 38 kutoka taasisi mbalimbali.
Amesema Kuwa kongamano hilo limekuwa hatua muhimu katika kuwakutanisha wadau na kuweka pamoja changamoto na mapendekezo yanayohusu haki za wanawake katika umiliki wa ardhi.
Miongoni mwa maeneo yaliyowasilishwa na mmoja wa washiriki yaliyowekwa katika makubaliano ya kongamano ni kuharakisha maboresho ya kisheria na kiutawala katika sekta ya ardhi, kuimarisha utekelezaji wa masuala ya ridhaa katika miamala ya ardhi, hususan ridhaa ya wanandoa, pamoja na kukabiliana na mila na desturi kandamizi zinazozuia wanawake kupata na kumiliki ardhi.
Washiriki pia wamependekeza kuimarisha mipango shirikishi ya matumizi ya ardhi na kuhakikisha masuala ya kijinsia yanazingatiwa katika vyombo vya maamuzi. Aidha, wameeleza umuhimu wa kuboresha upatikanaji wa takwimu za ardhi, ikiwemo katika maeneo ambayo yanatumiwa na wafugaji.
Naye Dkt. Monica Mhoja amesema kongamano hilo litakuwa likifanyika kila mwaka, huku kongamano lijalo likitarajiwa kufanyika jijini Arusha mwezi Agosti 2027.
Kongamano hilo limefanyika chini ya Kampeni ya “Linda Ardhi ya Mwanamke” kwa kaulimbiu “Imarisha Haki na Milki Salama za Ardhi na Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia Nchi kupitia Uongozi wa Wanawake wa Ngazi ya Jamii.”

