Agosti 10, 2026. Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya Yas imeshinda tuzo mbili katika Tuzo za TEHAMA 2026, ikiwemo ya Mtandao Bora wa Huduma za Intaneti Kitaifa (Best National ISP) kwa mwaka wa pili mfululizo.
Yas pia imeshinda tuzo ya TEHAMA kwa Uhifadhi wa Mazingira (ICT for Environmental Conservation), inayotambua matumizi ya teknolojia katika kuchangia juhudi za utunzaji wa mazingira na maendeleo endelevu.
Tuzo hizo zilitolewa usiku wa Agosti 9, 2026 katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, katika hafla iliyowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya TEHAMA na huduma za kidijitali. Mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb).
Akizungumzia ushindi huo, Afisa Mkuu wa Yas Business, Bw. Norman Kiondo, amesema kampuni hiyo itaendelea kuwekeza katika miundombinu na teknolojia ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi na kuwawezesha kutumia fursa zinazotokana na ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
“Intaneti imekuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku. Watu wanaitumia kufanya biashara, kufanya kazi, kujifunza, kupata huduma na kuwasiliana. Dhamira yetu ni kuendelea kujenga Mtandao wa Viwango unaowaunganisha Watanzania na kuwafungulia fursa zaidi za kidijitali popote walipo,” amesema Kiondo.
Amesema Yas inaona fahari kubwa kutambuliwa katika kipengele cha ‘Best National ISP’ kwa mwaka wa pili mfululizo tukitambua fika kuwa matumizi ya intaneti yanaendelea kuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku, kuanzia mawasiliano, elimu na burudani hadi biashara, ajira na upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa njia ya kidijitali.
Vilevile, kuibuka mshindi kwenye kipengele cha ‘ICT for Environmental Conservation’ kutaifanya Kampuni kuongeza msukumo kuendelea kutumia teknolojia ili kuendeleza juhudi za kuijenga Tanzania yenye maendeleo endelevu.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, mkakati wake ni kuendelea kuwa mshirika wa kidijitali wa Watanzania kwa kupanua huduma za mawasiliano na kuwezesha matumizi ya teknolojia katika maisha ya kila siku.
Tuzo za TEHAMA 2026 zimeandaliwa na Tume ya TEHAMA (ICTC) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kwa lengo la kutambua kampuni, taasisi na viongozi wanaochangia katika ubunifu, matumizi ya teknolojia na maendeleo ya sekta ya TEHAMA nchini.

