10 Agosti 2026, Dar es Salaam. Kampuni ya huduma za kifedha kidijitali, Mixx, imeshinda tuzo tatu katika Tuzo za TEHAMA 2026, ikiwemo nafasi ya kwanza katika kipengele cha Mobile Financial Services Innovation, huku Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Bi. Angelica Pesha, akitwaa tuzo ya Female ICT Leadership.

Mixx pia imeshika nafasi ya pili katika kipengele cha Digital Business Innovation, ikiwa ni kutambua matumizi ya teknolojia na ubunifu katika kurahisisha upatikanaji na matumizi ya huduma za fedha kidijitali.

Tuzo hizo zilitolewa usiku wa Agosti 9, 2026 katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, katika hafla iliyowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya TEHAMA na huduma za kidijitali. Mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb).

Katika kipengele cha Mobile Financial Services Innovation, Mixx ilishika nafasi ya kwanza kutokana na ubunifu wake katika kutumia teknolojia kurahisisha huduma za kifedha na kuzifikisha kwa Watanzania wengi zaidi.

Kupitia huduma zake, Mixx imeendelea kupanua matumizi ya huduma za kifedha kidijitali zaidi ya kutuma na kupokea fedha, kwa kuwawezesha wateja kuweka akiba, kupata mikopo na kufikia fursa mbalimbali za uwekezaji kupitia simu zao. Huduma hizo zinawapa Watanzania, wakiwemo wafanyabiashara wadogo, wakulima na makundi mengine katika jamii, njia rahisi zaidi ya kusimamia fedha zao na kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Kampuni hiyo pia ilishinda nafasi ya pili katika kipengele cha Digital Business Innovation, kinachotambua ubunifu kidigitali katika kuboresha biashara.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx, Bi. Angelica Pesha, alitunukiwa tuzo ya Female ICT Leadership, inayotambua mchango wa wanawake katika uongozi, ubunifu na maendeleo ya sekta ya TEHAMA nchini.

Akizungumzia ushindi huo, Pesha amesema tuzo hizo zinaipa Mixx msukumo wa kuendelea kuwekeza katika huduma zinazotumia teknolojia kupanua fursa za kifedha kwa Watanzania.

“Ushindi huu ni heshima kubwa kwetu na ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kuendelea kubuni huduma zinazojibu mahitaji ya wateja wetu. Tunataka teknolojia iendelee kuwa nyenzo inayorahisisha maisha na biashara za Watanzania kila siku, iwe ni katika kufanya malipo, kuweka akiba, kupata mikopo au kujenga fursa za uwekezaji,” amesema Pesha.

Amesema Mixx itaendelea kutumia teknolojia kuleta huduma za kifedha karibu zaidi na wananchi na kutoa suluhisho zinazowawezesha kusimamia fedha zao kwa urahisi na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.

Tuzo za TEHAMA 2026 zimeandaliwa na Tume ya TEHAMA (ICTC) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, kwa lengo la kutambua kampuni, taasisi na viongozi wanaochangia katika ubunifu, matumizi ya teknolojia na maendeleo ya sekta ya TEHAMA nchini.