NA DENIS MLOWE, IRINGA
MANISPAA ya Iringa imepokea rasmi magari mawili yenye thamani ya Sh milioni 240.6 kwa ajili ya kurahisisha usimamizi wa utekelezaji wa miradi ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji (TACTIC) inayotekelezwa katika manispaa hiyo.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika hafla fupi iliyohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamini Sitta, Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, wataalamu wa Manispaa, TARURA pamoja na wadau wanaohusika na utekelezaji wa mradi huo katika viwanja vya manispaa.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Sitta amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa kwa juhudi za kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku akiwataka wataalamu kuhakikisha miradi inayotekelezwa kupitia TACTIC inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Sitta amesema magari hayo yamenunuliwa na mkandarasi kwa ajili ya shughuli za usimamizi wa mradi na yamekabidhiwa kwa Mhandisi Msimamizi ili kurahisisha ufuatiliaji wa kazi katika maeneo mbalimbali ya mradi.
Amesema baada ya kukamilika kwa mradi, magari hayo yatabaki kuwa mali ya Serikali na kutumika katika shughuli nyingine za Serikali, hivyo akasisitiza umuhimu wa kuyatunza na kuyatumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Magari haya tunawakabidhi yakiwa mazuri na hali nzuri, yakiwa mapya kwa matumizi tunaomba yawe mazuri ili magari haya yaje kuwa na tija zaidi katika kazi zingine za Serikali,” alisema Sitta.
Aidha Sitta amemtaka Mshauri Elekezi wa mradi kusimamia kwa karibu kazi za mkandarasi ili kuhakikisha Serikali inapata thamani ya fedha na miradi inayokidhi viwango vilivyowekwa.
Mradi wa TACTIC katika Manispaa ya Iringa unahusisha ujenzi wa Soko la Kihesa, Ofisi ya Wahandisi pamoja na uboreshaji wa barabara za Mkimbizi-Bima, Mtwivila, Viziwi na Bontank zenye urefu wa jumla ya kilomita 5.26.
Kwa upande wake Mhandisi wa Manispaa ya Iringa, Rajabu Msangi alisema mradi huo ulianza Novemba 20, 2025 na unatarajiwa kukamilika Februari 11, 2027. Hadi sasa utekelezaji wake umefikia asilimia 20.5.
Alisema gharama ya kazi zinazofanywa na mkandarasi ni Sh bilioni 20.258, huku gharama ya Mshauri Elekezi ikiwa dola za Marekani 550,397.50.
Katika utekelezaji wa mradi huo, ujenzi wa barabara unahusisha ujenzi wa makalavati sita, ambapo matatu tayari yamekamilika, ujenzi wa mifereji, uwekaji wa lami, taa na alama za barabarani,ujenzi wa Ofisi ya Wahandisi unaendelea, huku katika Soko la Kihesa kazi ikiwa imefikia hatua ya ujenzi wa kuta.
Msangi alisema mradi huo umekumbana na changamoto kadhaa, ikiwemo mvua za Desemba hadi Machi 2026 zilizoathiri baadhi ya kazi za udongo na tabaka za barabara, pamoja na kuchelewa kupatikana kwa baadhi ya wataalamu na kutokuwapo kwa mitambo ya kutosha.
Hata hivyo, amesema mkandarasi amechukua hatua za kukabiliana na changamoto hizo kwa kupanga upya ratiba ya kazi na kuongeza kasi ya utekelezaji ili kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa.
Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, amesema utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya juhudi za kuboresha huduma na miundombinu katika Manispaa ya Iringa, akiwataka wadau wote kushirikiana kuhakikisha malengo ya mradi yanafikiwa.

