NA DENIS MLOWE, IRINGA
MKURUGENZI wa Manispaa ya Iringa, Zaina Mlawa, amezionya kampuni zinazofanya shughuli za usafi katika Manispaa za Bejom na Suma JKT, pamoja na wafanyakazi wa usafi kuzingatia maadili na uwajibikaji pindi wanapotekeleza majumuku yao ya kila siku.
Akizungumzia na kampuni hizo wakiambatana na wataalamu wa afya, usafi na mazingira, kwa lengo la kujadili changamoto zinazojitokeza katika huduma za usafi na kuchukua hatua za kuboresha mazingira.
Kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano huo umekuja kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na wananchi kupitia vyombo vya habari kuhusu baadhi ya changamoto katika ukusanyaji wa taka, pamoja na mwenendo na lugha zisizo na maadili zinazodaiwa kutumiwa na baadhi ya watendaji wa usafi wanapotekeleza majukumu yao.
Zaina Mlawa aliwataka wafanyakazi hao kuheshimu kazi zao, kuzingatia maadili na kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo, akisisitiza kuwa Manispaa haitakubali vitendo vinavyoweza kuichafua taswira ya Manispaa ya Iringa.
“Zingatieni maadili. Leo nataka tuambiane ukweli. Nataka mheshimu kazi yenu na kufuata maadili. Kama kuna mtu ana changamoto amewashinda nyie wazabuni, mtajeni hapa tumuondoe. Hatuwezi kukubali kufedheheshwa,” alisema Zaina.
Alisema lengo la kikao hicho si kulaumiana, bali kujenga ushirikiano utakaoifanya Manispaa ya Iringa kuwa mfano katika suala la usafi, ndani ya Mkoa wa Iringa, kitaifa na hata kimataifa.
“Tulikuwa na malalamiko ya wananchi wetu kuhusiana na kauli ambazo siyo njema, siyo nzuri, ambazo hazina maadili na hazina utii kwa jamii naamini tumejadiliana kwa kina pia niwapongeze kwa wale ambao tayari tumeshawachukulia hatua,” alisema.
Zaina pia aliwataka wafanyakazi kutambua umuhimu wa ajira walizonazo katika kipindi ambacho ajira ni changamoto kwa vijana wengi, akisisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kuzitendea haki nafasi aliyopewa kwa kufanya kazi kwa bidii na kwa nidhamu.
Alisema viongozi na watendaji wa mitaa wana wajibu wa kuwaelimisha wananchi kuhusu sheria na taratibu za utunzaji wa mazingira, ikiwemo muda na maeneo sahihi ya kuweka taka kwa ajili ya kukusanywa.
“Ni jukumu lako kuanza kuchukua hatua kwa kumuelimisha na kuchukua hatua stahiki umeona iko juu ya uwezo wako, njoo utuambie na sisi. Kwa sababu hakuna mwananchi ambaye yuko juu ya sheria. Ni lazima wote tutii sheria bila shuruti,” alisisitiza.
Aidha alieleza kuwa baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika ukusanyaji wa taka zinatokana na wananchi kuweka taka katika maeneo yasiyo sahihi au kuziweka siku nyingi kabla ya ratiba ya gari la taka kufika.
Alivitaka vyombo vya serikali za mitaa kuwaelimisha wananchi kuhusu siku maalum za ukusanyaji wa taka katika maeneo yao ili kuzuia taka kukaa muda mrefu na kusababisha uchafuzi wa mazingira.
Zaina pia alizitaka kampuni zinazohusika na ukusanyaji wa taka kuzingatia ratiba walizopewa na kuhakikisha taka zinaondolewa kwa wakati na endapo gari litapata hitilafu au changamoto nyingine inayozuia ukusanyaji wa taka, kampuni zinapaswa kutoa taarifa mapema ili Manispaa iweze kutafuta njia mbadala.
Alisema Manispaa inaweza kutumia magari au vifaa vilivyopo kwa ajili ya kusaidia maeneo yanayokabiliwa na changamoto, ili kuhakikisha taka hazikai kwa muda mrefu na kusababisha uchafuzi wa mazingira.
Katika hatua nyingine Zaina alisema Manispaa inaendelea na jitihada za kutengeneza vizimba maalumu vya kuhifadhia taka, hususan maeneo ya masoko, ili kuwezesha taka kuwekwa katika sehemu salama na kupunguza utupaji holela.
Pia alitoa rai kwa watendaji wa mitaa kuendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu utunzaji wa taka zenye majimaji, hususan katika maeneo ya machinjio ya kuku, ili kuzuia uchafu huo kuingia kwenye mifereji ya maji na kusababisha mazingira kuwa machafu.
Akizungumzia ukusanyaji wa ada za huduma ya uzoaji taka, Mkurugenzi huyo aliwataka watendaji wa serikali za mitaa kushirikiana na kampuni na wadau wanaohusika na makusanyo hayo ili kuongeza ufanisi wa huduma.
Alisema usafi wa Manispaa ni jukumu la pamoja linalohitaji ushirikiano kati ya serikali, kampuni zinazotoa huduma, watendaji wa mitaa na wananchi.
“Niombe tufanye kazi pamoja. Watendaji, hii ni sehemu ya makusanyo yetu tushirikiane na hawa wadau kwa sababu wanapokuja kwenye mtaa wako, shirikiana nao,” alisema na kusisitiza kuwa mafanikio katika usafi wa Manispaa yanategemea nidhamu, maadili, uwajibikaji na ushirikiano wa kila mdau, akisema lengo kuu ni kuhakikisha Manispaa ya Iringa inaendelea kuwa miongoni mwa maeneo safi na yenye mazingira bora kwa wananchi na wageni.
