Na Mwandishi Wetu, Dodoma

CHUO Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeweka wazi fursa 11 za uwekezaji zinazolenga kutumia ardhi ya chuo hicho kuanzisha miradi mbalimbali kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), hatua inayolenga kuongeza shughuli za kiuchumi na kuchochea maendeleo ya Dodoma.

Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, Teresia Mwaulambo kutoka Kurugenzi ya Mipango na Uwekezaji ya UDOM, amesema miradi hiyo imeandaliwa katika sekta mbalimbali na ipo tayari kwa wawekezaji wenye nia ya kushirikiana na chuo hicho.

Amesema miradi hiyo ni pamoja na Maduka Makubwa (Shopping Mall), Hoteli ya Nyota Tano na Kiwanja cha Golf (Hotel and Golf Resort), Kudurufu na Kuchapisha (UDOM Printing and Publishing Press), Uzalishaji wa Nishati ya Umeme wa Jua wa Megawati 100 (100 MW Solar Power Plant), pamoja na Kituo cha Mafuta na Gesi Asilia (Petrol Station & CNG).

Miradi mingine ni Kituo cha Matibabu na Madawa (Medical and Pharmaceutical Centre), Kituo cha Ubora wa Mapinduzi ya Viwanda ya Tano (Centre for the Fifth Industrial Revolution Excellence), Kituo cha Mikutano ya Kimataifa (International Convention Centre), Viwanja vya Michezo Mbalimbali (Multi-Sports Hub), Jengo la Sanaa na Ubunifu (Creative Arts and Design Complex) na Kituo cha Baoteknolojia (Biotechnology Centre).

Teresia amesema baadhi ya miradi hiyo imeandaliwa kwa kuzingatia ukuaji wa Dodoma na ongezeko la shughuli za kitaifa na kimataifa, hususan mahitaji ya hoteli, mikutano, huduma za biashara, burudani na miundombinu mingine inayohitajika katika mji unaokua kwa kasi.

Amesema Hoteli ya Nyota Tano na Kiwanja cha Golf pamoja na Kituo cha Mikutano ya Kimataifa ni miongoni mwa miradi inayotarajiwa kuwa na mchango mkubwa kutokana na kuongezeka kwa wageni wanaofika Dodoma kwa shughuli mbalimbali, ikiwemo mikutano ya kitaifa na kimataifa.

“Tunapokuwa na hoteli ya nyota tano ambayo inachukua watu wengi, halafu tukawa na ukumbi wa mikutano wa kimataifa, watu kutoka mikoa mbalimbali na nchi mbalimbali wanaweza kuja kufanya mikutano hapa, wakapata sehemu ya kulala na huduma nyingine zote zinazohitajika,” amesema.

Amesema uwepo wa miradi hiyo katika eneo moja utawarahisishia wawekezaji kwa kuwa UDOM tayari inamiliki ardhi yenye hati halali na eneo la kutosha kwa utekelezaji wa miradi hiyo, hivyo kuondoa changamoto ya kutafuta ardhi ambayo mara nyingi hukabili wawekezaji wanapotaka kuanzisha miradi mipya.

Kwa mujibu wa Teresia, fursa hiyo inatoa nafasi kwa wawekezaji kuingia Dodoma na kushirikiana na UDOM katika kuendeleza miradi yenye tija, huku chuo kikitarajia uwekezaji huo kuongeza shughuli za kiuchumi, ajira na huduma kwa jamii.

Amesema ushirikiano kati ya UDOM na sekta binafsi kupitia mfumo wa PPP utasaidia kutumia vizuri rasilimali za chuo hicho, hususan ardhi, na wakati huo huo kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ambayo inaweza kuwa na manufaa kwa chuo, wawekezaji na Taifa kwa ujumla.