NA DENIS MLOWE- DAR ES SALAAM
VICTORIA Group ambao ni waandaaji wa mbio za VG Fun Run 2026 wamesema maandalizi ya tukio hilo yamekamilika kwa asilimia 100 huku washiriki 250 wakitarajiwa kushiriki katika mbio hizo zitakazofanyika siku ya kesho Agosti 8, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya VG Fun Run, Isdori Msaki, alisema maandalizi yote muhimu yamekamilika na kila kitu kiko tayari kuhakikisha tukio hilo linafanyika kwa mafanikio.
Alisema washiriki watashiriki mbio za kilomita tano na kilomita 10, huku wale wasioweza kukimbia wakipata nafasi ya kushiriki mazoezi ya aerobics kama sehemu ya kuhamasisha afya na mtindo bora wa maisha.
“Tumekamilisha maandalizi kwa asilimia 100. Tunatarajia washiriki 250, huku hadi sasa watu 210 tayari wamethibitisha ushiriki wao. Tunaamini idadi hiyo itaongezeka siku ya tukio,” alisema Msaki.
Aliwashukuru wadhamini mbalimbali waliochangia kufanikisha tukio hilo akiwemo wanachama wa Victoria Group, Victoria Finance, Victoria Insurance Brokers, Mayfair Insurance, Elique, Heameda Hospital, IB Solution, CRDB Foundation , Melissa pamoja na Hill Water.
Msaki alisema Heameda Hospital itatoa huduma za afya kwa washiriki wote kupitia madaktari na wauguzi watakaokuwepo eneo la tukio ili kuhakikisha usalama wa washiriki wakati wote wa mbio.
Alisema IB Solution imechangia huduma za ubunifu wa michoro na usimamizi wa mitandao ya kijamii, huku CRDB Foundation ikiwa mmoja wa wadhamini wakuu waliowezesha maandalizi ya tukio hilo kufanikiwa.
Aliongeza kuwa Victoria Group imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na CRDB kwa zaidi ya miaka 26, jambo ambalo limeendelea kuimarisha ushirikiano katika shughuli mbalimbali za kijamii na maendeleo.
Msaki, washiriki wote wanatakiwa kufika eneo la tukio saa 12:00 asubuhi ambapo shughuli zitaanza kwa mazoezi ya kupasha mwili joto kabla ya kuanza rasmi kwa mbio.
Alisema mgeni rasmi wa tukio hilo atakuwa Mtendaji Mkuu wa CRDB Foundation, Tuli Mwambapa, ambaye anatarajiwa kuongoza uzinduzi wa mbio hizo kutokana na mchango wa taasisi hiyo katika kuunga mkono shughuli za kijamii.
Msaki alisema Victoria Group imeendelea kukua kwa zaidi ya miaka 26 ikiwa na wanachama 113, huku ikijumuisha familia zinazofanya jumla ya zaidi ya watu 700 wanaoshiriki shughuli mbalimbali za kijamii na maendeleo.
Aliongeza kuwa pamoja na wanachama wa Victoria Group, viongozi wa serikali, wafanyabiashara, wataalamu kutoka sekta binafsi pamoja na marafiki wa kundi hilo wanatarajiwa kushiriki katika mbio hizo.
Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki tukio hilo ambalo linalenga kuhamasisha mazoezi ya mwili, kuimarisha afya, kujenga urafiki na kuendeleza mshikamano katika jamii.
“Tunawakaribisha Watanzania wote kushiriki nasi. Mbali na kufanya mazoezi, tukio hili ni fursa ya kuimarisha afya, kukuza urafiki na kuendelea kujenga umoja katika jamii,” alisema Msaki.
