Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi,Ajira na Mahusiano Deus Sangu ( shati la njano) akimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Lindi Victoria Mwanziva akitoa maelezo kuhusu mradi wa ujenzi wa stendi ya Mtama unaotekelezwa na serikali kwa shilingi Bilioni 2.7 ikiwa ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka 2025.Waziri Sangu yuko Lindi kwa ziara ya kikazi .

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu alikagua mradi wa ujenzi wa barabara za halmashauri ya Mtama jana mkoani Lindi barabara yenye urefu wa mita 1,120 inayogharimu milioni 680.

Kasimba: Waziri wa Nchi ,Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Sangu akizungumza na wananchi wa Mtama wilaya ya Lindi jana alipokwenda kukagua miradi ya ujenzi wa barabara na stendi ambapo amewaeleza kuwa serikali ya Awamu ya Sita imefanikiwa kutoa Bilioni 13 kugharimia miradi mbalimbali ikiwa na lengo la kuboresha maisha ya wananchi.

( Picha OWM- KAM)

…………. 

Na OWM (KAM), Mtama – Lindi

Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kutekeleza kwa vitendo ahadi zake za maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Mtama, Mkoa wa Lindi, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 13 zimetolewa katika mwaka wa fedha 2025/26 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hatua ambayo imeelezwa kuleta tabasamu kwa wananchi.

Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwa fedha za Serikali katika Jimbo la Mtama, ikiwemo ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi na barabara, Agosti 6, 2026.

Sangu alisema fedha hizo zimeelekezwa katika miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa shule nne za sekondari kwa zaidi ya shilingi bilioni tatu, shule za awali na msingi kwa shilingi bilioni 1.2, vituo vya afya, stendi ya kisasa ya mabasi pamoja na jengo jipya la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Mtama.

Alisema ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi unaonesha dhamira ya Serikali ya kuboresha miundombinu ya huduma za usafiri, huku akiipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mtama kwa kutumia shilingi milioni 980 za mapato ya ndani kuanzisha mradi huo.

Waziri huyo alibainisha kuwa Serikali tayari imetenga shilingi bilioni moja katika bajeti ya mwaka 2026/27 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa stendi hiyo, fedha ambazo alisema zitaanza kutolewa katika kipindi kifupi kijacho ili mradi huo ukamilike kwa wakati.

Aidha, alisema Serikali imeendelea kuwekeza katika ujenzi wa barabara za lami ndani ya halmashauri hiyo, ambapo shilingi milioni 680 zimetengwa kujenga barabara yenye urefu wa mita 1,120 pamoja na kuweka taa za barabarani ili kuboresha mazingira ya biashara na usalama wa wananchi.

Sangu alisema kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wanaona matokeo ya maendeleo kupitia huduma bora na miundombinu inayogusa maisha yao ya kila siku.

Alisema kauli ya Rais Samia kwamba anatamani ifikapo mwaka 2030 aache tabasamu kwa Watanzania inaendelea kutimia kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa nchini, akieleza kuwa barabara za lami, majengo ya kisasa ya utawala na miradi mingine ni vielelezo vya dhamira hiyo.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Lindi Vijijini, Athuman Hongonyoko, alisema wananchi wa Mtama na Mkoa wa Lindi kwa ujumla wanaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, hususan ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi ambayo imekuwa kilio cha muda mrefu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva alimshukuru Waziri Sangu kwa kufanya ziara ya kukagua miradi katika halmashauri zote sita za mkoa huo kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan, akisema hatua hiyo imeongeza uwajibikaji na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Zuena Omary, alieleza kuwa pamoja na mafanikio hayo, mkoa huo bado unakabiliwa na changamoto ya wanyamapori waharibifu na migogoro kati ya wakulima na wafugaji, akiomba Serikali kuendelea kuimarisha uwezo wa wataalamu na upatikanaji wa vifaa vya kudhibiti tatizo hilo pamoja na kutenga maeneo maalumu kwa shughuli za kilimo na ufugaji.

Ziara ya Waziri Sangu ya siku sita mkoani Lindi imehitimishwa baada ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika wilaya za Kilwa, Liwale, Nachingwea, Ruangwa na Lindi, akiwa mlezi wa kiserikali wa mkoa huo kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi yenye tija kwa maendeleo na ustawi wa wananchi.