Mwakilishi kutoka kampuni ya Zawadi Agrovety ,Hawa Abdallah akizungumza na waandishi wa habari kuhusu huduma wanazotoa katika maonesho ya nanenane Njiro.

Mwakilishi kutoka kampuni ya Zawadi Agrovety ,Hawa Abdallah akitoa maelezo ya mbegu hizo kwa mkulima aliyefika kwenye banda hilo katika maonesho ya nanenane Njiro.
………
Na Happy Lazaro, Arusha.
KILIMO cha mboga mboga kimeelezwa kuwa moja ya sekta zenye uwezo mkubwa wa kuwaondoa vijana kwenye ukosefu wa ajira na kuwawezesha kujenga maisha bora kupitia uzalishaji wenye tija na matumizi ya mbegu bora.
Akizungumza katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Njiro mkoani Arusha, Mwakilishi wa kampuni ya Zawadi Agrovety, Hawa Abdallah, amesema kampuni hiyo inaendelea kutoa elimu kwa wakulima na vijana kuhusu matumizi ya mbegu bora zilizothibitishwa na Taasisi ya Udhibiti na Uthibitishaji wa Mbegu Tanzania (TOSCI) ili kuongeza mavuno na ubora wa mazao.
Amesema Zawadi Agrovety inasambaza mbegu za aina mbalimbali za mboga mboga, ikiwemo mchicha, mnavu, lettuce, Chinese cabbage, tikiti maji na matango, ambazo zimeonyesha matokeo mazuri kwa wakulima wanaozitumia katika maeneo mbalimbali nchini.
Hawa amesema kuwa,kilimo cha mboga mboga hakihitaji mtaji mkubwa kuanza, lakini kinaweza kumwezesha mkulima kupata kipato cha kila siku kupitia mauzo ya mazao kwa wateja wa majumbani, masokoni, migahawani na sehemu nyingine za biashara.
“Napenda kuwaasa vijana nchini kubadili mtazamo kuhusu kilimo na kukiona kama biashara yenye faida badala ya kusubiri ajira rasmi, kwani uzalishaji wa mboga mboga unaweza kuwa chanzo cha kujitegemea na kuboresha ustawi wa familia.”amesema Hawa.
Hawa ameongeza kuwa kupitia maonesho hayo kampuni hiyo imeendelea kuwafikia wakulima kwa kuwapatia elimu, ushauri wa kitaalamu na mbegu bora, hatua inayolenga kuongeza tija katika kilimo na kuchochea maendeleo ya sekta ya kilimo nchini.
Aidha ametoa wito kwa vijana kuchangamkia fursa hiyo ya kilimo.cha mbogmboga kwani hakina gharama na kuwa unaweza kulima sehemu ndogo na ukapata matokeo makubwa sana na hata wakati mwingine kuweza kuajiri vijana wengine.
