Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizindua mradi wa shule Mpya ya Awali na msingi katika Kijiji Cha Lagangabilili kitomgoji cha Mwankola wilayani Itilima mkoani Simiyu. Wa pili kulia ni Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akimkabidhi hati milki ya Ardhi Mkuu wa Chuo Cha VETA Bw. Deogratius Muzambele wakati alipokwenda kuzindua shule Mpya ya Awali na msingi katika Kijiji Cha Lagangabilili kitongoji cha Mwankola wilayani Itilima mkoani Simiyu.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo pamoja na Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha wakiwa katika picha ya pamoja na Wananchi walikabidhiwa hati milki za ardhi wakati alipokwenda kuzindua shule Mpya ya Awali na msingi katika Kijiji Cha Lagangabilili kitomgoji cha Mwankola wilayani Itilima mkoani Simiyu.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akimsikiliza mkazi wa Itilima Bw. Thomas Golea aliyewasilisha kero yake wakati wa uzinduzi wa shule Mpya ya Awali na msingi katika Kijiji Cha Lagangabilili kitongoji cha Mwankola wilayani Itilima mkoani Simiyu.

 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo pamoja na Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha wakiwa katika picha ya pamoja katika jengo la shule ya Mpya ya Awali katika Kijiji Cha Lagangabilili kitomgoji cha Mwankola wilayani Itilima mkoani Simiyu. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

………….. 

Na Munir Shemweta, Itilima

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, amepongeza hatua iliyofikiwa katika ujenzi wa Shule mpya ya Awali na Msingi Mwankola iliyopo Kijiji cha Lagangabilili, Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, huku akisisitiza kuwa elimu ni msingi muhimu wa maisha na maendeleo ya Taifa.

Dkt. Akwilapo amesema jamii inayowekeza katika elimu inaweka msingi imara wa maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho kwa kuwa elimu huwajengea watoto uwezo wa kujitambua, kupata maarifa na kujiandaa kushika nafasi mbalimbali za uongozi na kitaaluma.

Ametoa kauli hiyo Agosti 7, 2026 wakati wa ziara yake katika Kitongoji cha Mwankola, Kata ya Lagangabilili wilayani Itilima, ambako alikagua maendeleo ya mradi huo na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule hiyo.

Amesema wananchi wa Itilima wanapaswa kuendelea kuyapa umuhimu mkubwa masuala ya elimu na kuhakikisha watoto wanapata fursa ya kusoma katika mazingira bora, akieleza kuwa elimu ndiyo njia inayoweza kuwajengea vijana uwezo wa kuwa viongozi na wataalamu wenye mchango katika jamii.

uwekezaji unaofanywa na Serikali katika miundombinu ya elimu unapaswa kuungwa mkono na wananchi, hususan wazazi na walezi, kwa kuhakikisha watoto wanahudhuria masomo na kupata mahitaji muhimu yatakayowawezesha kujifunza vizuri’’. Amesema Dkt Akwilapo

Akiwa katika eneo la mradi huo, Waziri Akwilapo aliwahimiza wazazi kutambua kuwa wao ni sehemu muhimu ya mafanikio ya elimu ya watoto wao, hivyo wanapaswa kushirikiana na Serikali na viongozi wa shule katika kuboresha mazingira ya ujifunzaji.

Pamoja na hilo, amesisitiza umuhimu wa wanafunzi kupata chakula shuleni, akibainisha kuwa upatikanaji wa chakula ni moja ya mambo yanayoweza kumsaidia mtoto kuwa katika mazingira mazuri ya kujifunza na kufuatilia masomo.

Amesema jitihada za kujenga madarasa na shule mpya zinapaswa kwenda sambamba na ushiriki wa wazazi katika ustawi wa wanafunzi ili uwekezaji unaofanywa na Serikali katika sekta ya elimu uweze kutoa matokeo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa wa Simiyu Mhe. Anamringi Macha amesema mkoa wake umepiga hatua katika sekta kubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya na miundombinu.

Ameeleza kuwa hatua hizo zinatokana na juhudi kubwa zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwaletea maendeleo wananchi.

Ziara hiyo ni sehemu ya mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kuwapeleka mawaziri katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali iliyoahidiwa kwa wananchi wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipokuwa akiomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Kupitia ziara hizo, Serikali inafuatilia hatua za utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na changamoto zinazoweza kujitokeza ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma na miradi iliyokusudiwa kwa wakati.