Dodoma

Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda, Agosti 06,2026 ametembelea banda la Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika Maonesho ya 88 ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Samuel Malecela, jijini Dodoma.

Akiwa katika banda hilo, Mhe. Pinda alipokea maelezo kuhusu huduma zinazotolewa na VETA, ikiwemo mafunzo ya ufundi stadi, ubunifu wa teknolojia mbalimbali pamoja na fursa zinazowawezesha vijana kujiajiri na kuchangia maendeleo ya uchumi wa taifa.

Pia alitembelea sehemu mbalimbali za maonesho ndani ya banda hilo na kujionea kazi za ubunifu zinazozalishwa na wanafunzi na wakufunzi wa VETA, huku akipongeza juhudi zinazofanywa na taasisi hiyo katika kuwaandaa Watanzania wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira.

VETA inaendelea kutumia Maonesho ya Nanenane kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kozi mbalimbali zinazotolewa katika vyuo vyake, pamoja na kuhamasisha vijana na makundi mengine kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi kwa ajili ya kujenga taifa lenye wataalamu wenye ujuzi.