Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuimarisha nafasi ya Tanzania katika kuchochea mageuzi ya kiuchumi barani Afrika baada ya nchi kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa siku mbili wa Wanahisa wa Africa50 pamoja na Jukwaa la Miundombinu Afrika, uliomalizika jijini Dar es Salaam Agosti 6, 2026.

Mkutano huo, uliofunguliwa rasmi na Rais Samia, uliwakutanisha Wakuu wa Nchi, Mawaziri, viongozi wa taasisi za umma na binafsi, pamoja na wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kujadili mikakati ya kuharakisha ujenzi wa miundombinu yenye kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye ya bara hilo.

Katika majadiliano hayo, wataalamu na wasomi wabobezi walichambua njia mbalimbali za kuongeza upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya miundombinu. Walisisitiza kuwa Afrika ina rasilimali za kutosha, lakini zinahitaji kusimamiwa kwa mikakati madhubuti ili ziwe chachu ya maendeleo na mageuzi ya kiuchumi.

Washiriki wa mkutano huo walieleza kuwa mafanikio katika sekta ya miundombinu yanategemea uwepo wa mifumo imara ya kisiasa, sera thabiti, ushiriki wa sekta binafsi, mfumo wa sheria unaolinda maslahi ya wadau, pamoja na kuandaa miradi inayovutia uwekezaji na kupata ufadhili kwa urahisi.

Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alisema miundombinu ndiyo msingi wa mageuzi ya kiuchumi barani Afrika. Alisisitiza kuwa miundombinu haipaswi kutumika kwa ajili ya kusafirisha bidhaa pekee, bali pia iwe chachu ya kuzalisha ajira, kukuza biashara na kuendeleza ujuzi, hususan kwa vijana.

Dkt. Kikwete pia alihimiza nchi za Afrika kuwekeza zaidi katika elimu bora, akibainisha kuwa ifikapo mwaka 2050, robo ya watu wote wenye umri wa kufanya kazi duniani watakuwa wanaishi barani Afrika. Alieleza kuwa uwekezaji katika elimu ni njia muhimu ya kujenga nguvu kazi yenye tija na kupunguza hatari ya migogoro ya kijamii.

Mkutano wa Wanahisa wa Africa50 ulifanyika chini ya kaulimbiu, “Miaka 10 ya Mafanikio: Kutoka Maono hadi Utekelezaji,” ukilenga kuhamasisha upatikanaji wa mitaji kupitia ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuharakisha ujenzi wa miundombinu na kuchochea maendeleo endelevu barani Afrika.