Mkurugenzi wa Vodacom Business Nguvu Kamando, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu msimu mpya wa msafara wa Nyerere Cycling Tour (zamani Twende Butiama) utakaozinduliwa mnamo mwezi wa kumi ukiambatana na mashindano ya mbio za Vodacom Coastal Classic.
Wadau na Washiriki wa msafara wa mbio za Nyerere Cycling Tour (zamani Twende Butiama) wakipiga makofi kama ishara ya kufurahia ujio wa mashindano ya mbio za Vodacom Coastal Classic.
Mwanzilishi wa Msafara wa Mbio za Twende Butiama, Gabriel Landa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu msimu mpya wa msafara wa Nyerere Cycling Tour (zamani Twende Butiama) utakaozinduliwa mnamo mwezi wa kumi.
Wadau wa msafara wa Cycling tour (zamani Twende Butiama) wakisikiliza kwa makini kuhusu msimu mpya wa msafara huo na ujio wa Mashindano ya Vodacom Coastal Classic utakaozinduliwa mnamo mwezi wa kumi mwaka huu.
……………
* Twende Butiama yabadilishwa jina kuwa Nyerere Cycling Tour
* Vodacom Coastal Classic yazinduliwa kwa mbio za kilomita 109
*Mashindano ya kwanza yatafanyika Oktoba 4, 2026 kutoka Dar es Salaam hadi Bagamoyo
Dar es Salaam, Agosti 6, 2026: Katika hatua muhimu ya kukuza mchezo wa baiskeli nchini, Vodacom Tanzania Plc kwa kushirikiana na Chama cha Baiskeli Tanzania (CHABATA), imetangaza rasmi kubadilishwa kwa jina la msafara wa baiskeli wa Twende Butiama na kuwa Nyerere Cycling Tour, sambamba na uzinduzi wa mashindano mapya ya Vodacom Coastal Classic, yatakayohusisha mbio za kilomita 109 kwa lengo la kuiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa ya mashindano ya baiskeli.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016, msafara huo umekuwa ukiendeleza urithi wa Mwalimu Julius K. Nyerere kwa kuboresha mazingira ya elimu kupitia ujenzi wa madarasa, miundombinu ya vyoo na utoaji wa vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuhakikisha kila mtoto anapata fursa sawa ya kujifunza.
Hadi sasa, msafara huo umefikia zaidi ya shule 107 na kuboresha maisha ya wanafunzi zaidi ya 75,000 kupitia ujenzi wa mazingira bora na jumuishi ya kujifunzia.
Vodacom Tanzania Foundation ilianza kushirikiana na CHABATA kufadhili msafara huo miaka minne iliyopita, ambapo umeendelea kukua kwa kasi na kuvutia washiriki kutoka Tanzania, Afrika Mashariki na mataifa mengine duniani. Msafara wa mwaka huu utafanyika kuanzia Oktoba 5 hadi 14, 2026, ukianzia Bagamoyo hadi Butiama.
Kwa mujibu wa waandaaji, kuanzia mwaka huu msafara huo utajulikana rasmi kama Nyerere Cycling Tour, hatua inayolenga kuuenzi urithi wa Mwalimu Nyerere na wakati huo huo kuujenga kuwa mashindano ya kimataifa ya baiskeli.
Sambamba na mabadiliko hayo, Vodacom Tanzania na CHABATA wamezindua mashindano ya Vodacom Coastal Classic, yatakayofanyika kwa mara ya kwanza Jumapili, Oktoba 4, 2026, yakihusisha mbio za kilomita 109 kwa wanaume na wanawake.
Mbio hizo zitaanzia Dar es Salaam, kupita Makurunge mkoani Pwani na kumalizikia katika eneo la kihistoria la Old Boma, Bagamoyo. Baada ya uzinduzi wake, mashindano hayo yatafanyika kila mwaka katika Jumapili ya kwanza ya mwezi Oktoba.
Washiriki zaidi ya 400 kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali duniani wanatarajiwa kushiriki katika mbio hizo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Vodacom Business, Nguvu Kamando, amesema lengo ni kukuza mchezo wa baiskeli na kuwapa fursa Watanzania wenye vipaji kushindana katika viwango vya kimataifa.
“Tunataka kukuza mchezo huu. Kila siku tunaona waendesha baiskeli kwenye barabara zetu. Hakuna sababu kwa nini vipaji vya Tanzania visitambuliwe kimataifa. Wanachohitaji ni vifaa na mafunzo sahihi, na Vodacom Coastal Classic inalenga kuwapa fursa hiyo,” amesema Kamando.
Kwa upande wake, Mwanzilishi wa Nyerere Cycling Tour, Gabriel Landa, amesema msafara huo umekuwa zaidi ya safari ya baiskeli kwani umeendelea kubeba maono ya Mwalimu Nyerere ya usawa na fursa kwa kila Mtanzania.
Nyerere Cycling Tour, ambayo awali ilijulikana kama Twende Butiama, inalenga kuenzi urithi wa Mwalimu Julius K. Nyerere kwa kuhamasisha upatikanaji wa elimu bora na jumuishi nchini. Kupitia mpango huo, zaidi ya shule 107 zimefikiwa na wanafunzi zaidi ya 75,000 wameendelea kunufaika na uboreshaji wa mazingira ya kujifunzia, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa, vyoo na utoaji wa vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
