HALMASHAURI ya Manispaa ya Ilemela imevuka lengo la ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha 2025/2026 baada ya kukusanya Sh bilioni 16.60, sawa na asilimia 101 ya makadirio ya bajeti ya Sh bilioni 16.46.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ummy Wayayu, alisema hayo leo alipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za halmashauri kwa kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026. Alisema mafanikio hayo yametokana na kuimarika kwa usimamizi wa ukusanyaji wa mapato, matumizi ya mifumo ya kidijitali na ushirikiano wa wananchi katika kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi na tozo mbalimbali.
Wayayu alisema mafanikio ya ukusanyaji wa mapato yameiwezesha halmashauri kutekeleza miradi ya maendeleo yenye thamani ya Sh bilioni 47.39 katika kipindi hicho. Alifafanua kuwa kati ya fedha hizo, Sh bilioni 4.24 zilitokana na mapato ya ndani huku Sh bilioni 43.16 zikitolewa na Serikali Kuu kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Alibainisha kuwa fedha hizo zimeelekezwa katika sekta za utawala, afya, elimu ya msingi, elimu ya sekondari na miundombinu, ambapo sehemu kubwa imeelekezwa katika miradi ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu kupitia programu ya TACTIC, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuboresha huduma kwa wananchi.
Aidha, Wayayu alisema Halmashauri itaendelea kuimarisha vyanzo vya mapato, kuongeza uwazi katika usimamizi wa fedha za umma na kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na huduma bora pamoja na thamani ya fedha zinazokusanywa.

