Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu ya barabara kwa kuacha vitendo vya uharibifu vinavyoongeza gharama za matengenezo na kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara.
Akitembelea banda la Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela jijini Dodoma, Dkt. Msonde alisema Serikali inaendelea kutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya matengenezo ya barabara ili kuhakikisha zinabaki katika hali nzuri na kuendelea kuhudumia wananchi pamoja na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Alisema pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika alama za barabarani, taa za kuongozea watumiaji wa barabara na miundombinu mingine ya usalama, baadhi ya wananchi wameendelea kujihusisha na vitendo vya uharibifu kama kung’oa taa na kuharibu alama za barabarani, hali inayoongeza gharama za matengenezo na kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara.
Aidha, aliwataka wananchi kuheshimu hifadhi za barabara kwa kuepuka kuvamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya upanuzi wa barabara na kufanya shughuli za biashara ndani ya hifadhi hizo, akieleza kuwa matumizi yasiyo sahihi ya maeneo hayo huchelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuongeza gharama za Serikali.
Dkt. Msonde alisisitiza kuwa barabara ni mali ya Watanzania wote na kwamba mafanikio ya Serikali katika kuhakikisha miundombinu hiyo inabaki salama na inapitika wakati wote yanategemea ushirikiano wa wananchi katika kuilinda, hivyo kulinda thamani ya fedha za umma na kuhakikisha miundombinu hiyo inaendelea kuhudumia kizazi cha sasa na kijacho.
