
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wakiwa kwenye mkutano na Waandishi wa Habari kufuatia Ziara Rasmi ya Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Ikulu Jijini Dar es Salaam, tarehe 06 Agosti, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni wakishuhudia utiaji saini Hati ya Makubaliano kuhusu mapendekezo ya kuendeleza Tanga kama Kituo cha Nishati cha Kikanda katika viwanja vya Ikulu, jijini Dar es Salaam, tarehe 06 Agosti, 2026. Hati hiyo ya Makubaliano imesainiwa kati ya Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC) chini ya Mkurugenzi Mtendaji Bw. Mussa Makame, Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) chini ya Mkurugenzi Mtendaji Bi. Proscovia Nabbanja pamoja na Kampuni ya Biashara ya Mafuta na Nishati ya Vitol ya Bahrain, chini ya Mkurugenzi Mtendaji wake Tom Baker.

Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini Mhe. Dkt. Musenero Masanza wa Uganda akizungumza kwenye mkutano wa Waandishi wa Habari baada ya hafla ya utiaji saini Hati ya Makubaliano kuhusu mapendekezo ya kuendeleza Tanga kama Kituo cha Nishati cha Kikanda ulioshuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Ikulu, jijini Dar es Salaam, tarehe 06 Agosti, 2026.



NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, wameshuhudia hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) inayolenga kuendeleza mkoa wa Tanga kuwa Kituo cha Nishati cha Kikanda. Hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam, Agosti 6, 2026.
Makubaliano hayo yamesainiwa na Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC), likiwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Bw. Mussa Makame; Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC), iliyowakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji, Bi. Proscovia Nabbanja; pamoja na Kampuni ya Vitol Bahrain, iliyowakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wake, Tom Baker.
Akizungumza leo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla hiyo iliyohudhuriwa na viongozi hao wakuu wa nchi, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema hatua hiyo ni kimkakati katika kuimarisha sekta ya nishati na kukuza uchumi wa Afrika Mashariki.
Mhe. Ndejembi amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuvutia uwekezaji unaozidi dola za Marekani bilioni 20, huku ukiongeza thamani ya rasilimali za mafuta katika ukanda huo.
Mhe. Ndejembi amesema makubaliano hayo yanaonyesha uwezo wa Tanzania na Uganda kushirikiana kama washirika wa kimkakati katika kuandaa, kufadhili na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo yenye manufaa ya pamoja kwa wananchi wa nchi zote mbili.
Aidha, ameeleza kuwa ushirikiano huo umejengwa juu ya mafanikio ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), wenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni sita, ulioanzishwa mwaka 2017 kwa ushirikiano wa Tanzania, Uganda na wadau wengine.
Amesisitiza kuwa Tanga imechaguliwa kutokana na ubora wake wa kiufundi, kiuchumi, kimazingira pamoja na nafasi yake muhimu ya kimkakati katika Afrika Mashariki.
Waziri Ndejembi ameongeza kuwa lengo la hatua hiyo si kusafirisha mafuta ghafi pekee, bali kujenga uchumi unaoongeza thamani ya rasilimali hizo kupitia shughuli za usafishaji wa mafuta, uhifadhi, biashara, usafirishaji, maendeleo ya viwanda, uundaji wa ajira na kukuza biashara ya kikanda.
Amesema mpango huo unatekeleza maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanga kuwa kitovu cha mafuta na nishati kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
