Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya Nanenane Nyamhongoro Jijini Mwanza ikiwa imesalia siku moja maonesho hayo kutamatika.
Na. Hellen Mtereko,Mwanza
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewashauri wananchi kutumia watoa huduma wenye leseni za EWURA pale wanapotaka kununua bidhaa hatua itakayosaidia kuepukana na changamoto mbalimbali ikiwemo majanga ya moto.
Ushauri huo umetolewa leo Agosti 07, 2026 na Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Nyirabu Musira alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye banda lao lililopo kwenye maonesho ya Nanenane Kanda ya Ziwa Magharibi yanayoendelea viwanja vya Nyamhongoro Wilayani Ilemela mkoani Mwanza.
Amesema Athali za kutumia watoa huduma ambao hawana leseni ni pamoja na kununua mitungi ambayo haijahakikiwa hivyo inaweza kuwa inavuja na kusababisha mlipuko ndani ya nyumba sanjari na kupata bidhaa ambayo iko chini ya kiwango.
Amesema athali nyingine ya kutumia watoa huduma ambao hawana leseni ni kukosa fidia pindi mtumiaji anapopata majanga.
“Kwa mfano unapoenda kununua mtungi wa gesi kwa mtu asie kuwa na leseni hata mzani wa kupimia anakuwa hana,lakini huyu mwenye leseni ya kutoka ewura anazijua taratibu zote hivyo atakuwa na mzani wa kupimia na atakuwa anauza mitungi ambayo imefunikwa vizuri na leseni yake itakuwa inaonekana kwenye eneo lake la biashara”, Amesema Musira
Aidha, ametoa rai kwa wafanyabiashara wanaouza bidhaa za nishati na maji kuwa na leseni kutoka EWURA ili waepukane na kufanya biashara kiholela.
