Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA), Profesa William Palangyo, amewakaribisha wananchi kutembelea banda la taasisi hiyo katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni jijini Dodoma, ili kujifunza kuhusu fursa mbalimbali za elimu, ujasiriamali na matumizi ya teknolojia katika kilimo na biashara.

Profesa Palanjo amesema TIA imeleta wataalamu na wanafunzi wake ili kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji na wafanyabiashara kuhusu uhasibu, utunzaji wa fedha, utunzaji wa kumbukumbu, masoko, ugavi pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika shughuli za uzalishaji na biashara.

Amesema moja ya vivutio vikubwa katika banda la TIA ni ubunifu wa wanafunzi kutoka kampasi za Mwanza na Kigoma ambao wameunda mifumo ya kidijitali inayolenga kutatua changamoto zinazowakabili wakulima na wafanyabiashara.

“Lengo letu si kuwafundisha wanafunzi wapate ajira pekee, bali kuwajengea uwezo wa kujiajiri kupitia ubunifu. Ndiyo maana tumeanzisha kitengo maalumu kinachowasaidia kubuni teknolojia na biashara zinazotatua changamoto za jamii,” amesema Profesa Palanjo.

Ameongeza kuwa TIA imeingiza matumizi ya teknolojia na akili mnemba (Artificial Intelligence) katika mitaala yake ili wanafunzi waweze kubuni suluhisho zinazokidhi mahitaji ya soko na kuchangia maendeleo ya sekta mbalimbali za uchumi.

Mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa TIA Kampasi ya Mwanza, Pasco Sabuni Shija, amesema amebuni mfumo wa mizani ya kidijitali unaotumia nishati ya jua (solar) na umeunganishwa na risiti za EFD pamoja na teknolojia ya akili mnemba ili kuboresha ununuzi wa pamba na mazao mengine.

Amesema mfumo huo unamwezesha mkulima kupata uzito sahihi wa mazao yake, kupokea risiti na ujumbe mfupi wa simu mara baada ya mauzo, huku ukitoa taarifa za bei ya soko kwa wakati halisi na kupunguza udanganyifu uliokuwa ukitokea kwenye mizani ya kawaida.

“Kupitia mfumo huu, mkulima anapata haki yake kwa sababu mizani haiwezi kuchezewa. Serikali pia inapata taarifa sahihi kwa wakati na wafanyabiashara wanafanya kazi kwa uwazi zaidi,” amesema Pasco.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa mwaka wa pili wa TIA Kampasi ya Kigoma, Daud Temaunji, amesema amebuni mfumo wa BizPower unaowawezesha wafanyabiashara, wakulima na wajasiriamali kusimamia biashara zao kwa njia ya kidijitali wakiwa mahali popote.

Amesema mfumo huo unawezesha mtumiaji kuona taarifa za mauzo, manunuzi, bidhaa zilizopo stoo na taarifa nyingine muhimu kupitia simu au kompyuta, huku ukiwa na uwezo wa kufanya kazi hata pasipo huduma ya intaneti.

Daud amesema ubunifu huo unalenga kuwasaidia wafanyabiashara kufanya maamuzi kwa haraka, kuboresha usimamizi wa biashara na kuongeza ufanisi katika shughuli zao za kila siku.