Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa Nyirabu Musira akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya Nane nane Jijini Mwanza

Na Hellen Mtereko,Mwanza

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewahamasisha wawekezaji kujenga vitio vya mafuta vijijini huku ikieleza namna gharama ya maombi ya leseni ilivyopungua kutoka milioni tano hadi milioni moja kwa wawekezaji wa maeneo ya vijijini.

Akizungumza Agosti 03, 2026 na waandishi wa habari kwenye maonesho ya Nane nane yanayofanyika katika uwanja wa Nyamhongoro Jijini Mwanza, Meneja wa EWURA Kanda ya ziwa, Nyirabu Musira amesema lengo la kufanya hivyo ni kuondoa biashara holela ya uuzaji wa mafuta kwenye maeneo hayo.

Amesema maeneo mengi ambayo hayana vituo vya mafuta kumekuwa na mfumuko wa biashara isiyo halali ya uuzaji wa mafuta kwenye vichupa na vidumu.

“Hiyo ni hatari sana kwani bidhaa yotote ya petroli ni kilipuzi na hatari kwa mazingira”,

Amesema miundo mbinu ambayo anapaswa kuijenga siyo lazima ambayo iko kwenye vituo vya mjini, kwa vijijini anaweza akawa na kituo cha mafuta chenye pampu moja na anaweza akawa na kituo cha mafuta kinachouza bidhaa moja na EWURA wakampa leseni ili aweze kuhudumia kwenye maeneo.

Aidha, ameongeza kuwa lile takwa linalohusina na upatikanaji wa cheti cha mazingira kwa maeneo ya vijijini anauwezo wa kuonana na maafisa mazingira wa Halmshauri husika na wakampa kibali ambapo akienda EWURA wanakitambua na kumpa leseni.

Mwisho aliwakaribisha wananchi kufika kwenye Banda lao lililopo kwenye maonesho ya Nane nane Nyamhongoro kwaajili ya kupata elimu zaidi.