Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Clement Sangu akikagua mradi wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi iliyopo Kilwa Masoko, Mkoani Lindi wakati wa ziara ya kikazi ya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo mkoani humo, leo Agosti 3, 2026. Jumla ya Bilioni 225 kati ya 280 tayari zimetolewa na Serikali kutekeleza mradi huo utakaowezesha ajira 300 za moja kwa moja na zingine 30,000 utakapokamilika.

Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Clement Sangu (aliyekaa) akikagua chumba maalum cha kamera za usalama na mifumo ya mawasiliano alipofanya ziara katika bandari ya Uvuvi iliyopo Kilwa Masoko, mkoani Lindi wakati wa ziara ya kikazi ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo leo Agosti 3, 2026.

Na. OWM (KAM) – Kilwa, Lindi

Vijana mkoani Lindi amewahimiza kuchangamkia fursa zitakazotokana na kukamilika kwa Mradi wa Kimkakati wa Bandari ya Uvuvi ya Kilwa ikiwemo ajira, biashara na masoko ya mazao ya uvuvi, ili kuchochea ukuaji wa uchumi na maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu wakati akizungumza na wananchi wa Kilwa Masoko mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa bandari ya uvuvi iliyojengwa na serikali.

Mhe. Sangu amesema kuwa mradi huo ni fursa muhimu kwa wananchi kupata ajira akitaja jumla ya ajira 30,000 ambazo zitapatikana mara ujenzi utakapokamilika na kusema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuona uchumi wa buluu ukichangia uchumi wa taifa.

” Kupitia bandari hii tumeona zaidi ya ajira 30,000 zitaenda kuzalishwa kwa kundi la vijana na wanachi wengine kutokana na bandari kuwa na uzalishaji wa zaidi ya tani 60,000 za samaki watakaovuliwa kwa mwaka” amesema Waziri Sangu.

Katika hatua nyingine Waziri Sangu amesema ujenzi wa bandari ya Kilwa ni utekelezaji wa Dira 2050 ambayo inaelekeza sekta binafsi kuchangia ukuaji wa uchumi ambapo serikali inakusudia kuzalisha ajira zaidi ya milioni nane (8).

Vile vile, ameongeza kuwa sekta ndogo ya uvuvi kwa sasa inachangia asilimia 2.2 ya pato la taifa ambapo lengo la Dira ya 2050 ni kufikia asilimia 9.8 .

Akiwasilisha taarifa ya mradi, Msimamizi wa mradi huo Mhandisi George Kwandu toka Wizara ya Mifugo na Uvuvi amesema ujenzi wa bandari ya uvuvi Kilwa Masoko umefikia asilimia 100 ambapo jumla ya shilingi bilioni 225 kati 280 zimetolewa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Kadhalika, amesema mradi huo umezalisha ajira 1,270 zilipatikana wakati wa ujenzi wa mradi huku ajira za moja kwa moja 300 zikitarajiwa wakati wa utekelezaji wa mradi na pia zaidi ya ajira 30,000 zitapatikana kipindi chote za mradi huo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mohamed Nyundo ameshukuru Serikali kwa kuona fursa ya bandari ya Kilwa Masoko na kuamua kutekekeleza mradi huo wa kimkakati ambao utakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa mkoa huo na taifa kwa ujumla.

“Kilwa Masoko tayari imeanza kazi ya kuelimisha vijana kupitia makongamano ili watambue fursa za kiuchumi zitakazotokana na mradi huu wa bandari ya uvuvi,” amesema

Naye, Mbunge wa Kilwa Kusini Mhe. Hasnain Dewji amesema kukamilika kwa mradi huo wa bandari ya uvuvi kutavutia wafanyabiashara katika sekta ya uvuvi ambapo hadi sasa nchi mbalimbali ikiwemo Somalia, Kenya na Msumbiji tayari zimeonesha utayari wa kuja kutumia bandari hiyo.

Mbunge huyo pia, amesema manufaa mengine ya kukamilika kwa mradi huo ni kuongezeka kwa mapato ya ndani ya halmashauri kutoka shilingi Bilioni 10 za sasa hadi Bilioni 25.

Waziri Sangu ameanza ziara ya kikazi ya siku tano (5) ya kukakagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali pamoja na kuzungumza na wananchi wa Mkoa wa Lindi.