Afisa kilimo kutoka Bodi ya Pamba Tanzania Dotto Ntumba akionesha baadhi ya vitu ambavyo wanavitumia kutolea elimu katika maonesho ya Nanenane Jijini Mwanza
Na Hellen Mtereko,Mwanza
Bodi ya Pamba Tanzania imeendelea kutanua wigo wa kutoa elimu kwa wadau sanjari na kuwajengea uelewa wa mambo mbalimbali yanayosaidia ukuaji wa zao hilo.
Hayo yamebainishwa jana Agosti 02, 2026 na Afisa kilimo kutoka Bodi ya Pamba Tanzania, Dotto Ntumba wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho ya Nanenane yanayofanyika katika uwanja wa Nyamhongoro Jijini Mwanza.
Amesema kwa sasa wameandaa sehemu kuu mbili kwaajili ya kutoa elimu ambapo moja ni eneo la shamba ambako wanawaeleza wadau kuhusu teknolojia mbalimbali ambazo zimefanyiwa utafiti zitakazo saidia mkulima kupata tija kwenye kilimo cha Pamba.
Pia ameeleza kuwa wanavifaa mbalimbali ikiwemo vya kupulizia sumu mashambani,ndege nyuki ambayo inarahisisha upuliziaji wa sumu mashambani kwa wakulima wenye mashamba makubwa.
Ameeleza kuwa katika maonesho hayo wanawaonesha wadau mnyororo mzima wa thamani wa zao la Pamba ili waweze kuona fursa za kiuchumi zilizoko kwenye zao hilo.
“Tunabidhaa ambazo tunaonesha ikiwemo Pamba mbegu ambayo inatoka kwa mkulima,mkulima anapopata pamba mbegu anamuuzia mwenye kiwanda cha kuchambua Pamba na yule anayechambua Pamba anapata bidhaa kuu mbili mbegu pamoja na nyuzi ambapo kunakiasi kinarudi shambani kwaajili ya kupandwa na nyuzi zinaenda kwa mtengeneza nguo”, Amesema Ntumba
Aidha, amesema mbegu zinazobaki zinakamuliwa mafuta na baada ya kukamua wanapata bidhaa nyingine kama mashudu,sabuni pamoja na bidhaa zingine zinazoambatana na shughuli hiyo.
Mwisho alieleza asilimia zaidi ya 30 ya pamba inatumika hapa nchini na hii ni kutokana na viwanda vingi vya nguo kufufuliwa na kujengwa hatua inayosaidia kuongeza thamani ya zao la pamba

