Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma 

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema Serikali itaendelea kuimarisha sekta ya ushirika kwa kuhakikisha vyama vya ushirika vinaendeshwa kwa weledi, uwazi na uwajibikaji ili viwe chachu ya maendeleo ya wananchi na uchumi wa Taifa.Akizungumza August 03,2026 katika Siku Maalum ya Ushirika ndani ya Maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane 2026 yanayofanyika Viwanja vya John Malecela, Nzuguni Dodoma, Dkt. Nchimbi amesema Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) inapaswa kuendelea kusimamia vyama vya ushirika na kutoa miongozo ya kitaalamu itakayoongeza ufanisi wa sekta hiyo.

Amesema Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (COASCO) linapaswa kuimarisha ukaguzi ili kuhakikisha fedha za vyama vya ushirika zinatumika kwa nidhamu na kuchukua hatua dhidi ya ubadhirifu.

“Ushirika unaozingatia uadilifu hujenga imani kwa wanachama na wawekezaji, jambo linalochochea ukuaji wa sekta hiyo,” amesema Dkt. Nchimbi 

Amebainisha kuwa kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu” inalenga kuongeza uwazi, uwajibikaji na kupambana na vitendo vinavyoweza kudhoofisha maendeleo ya vyama vya ushirika nchini.

Aidha, ameielekeza Wizara ya Kilimo kupitia TCDC kuhakikisha sekta ya ushirika inaendana na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kwa kuifanya kuwa na mwelekeo wa kibiashara na kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa.Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel  Chongolo, amesema Serikali itaendelea kuweka mikakati ya kuimarisha sekta ya ushirika ili iwe na mchango mkubwa katika kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, akionya kuwa hatua stahiki zitachukuliwa dhidi ya wanaokiuka misingi na taratibu za uendeshaji wa vyama vya ushirika.

Naye, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa TCDC, Dkt. Benson Ndiege, amesema zaidi ya Watanzania 155,000 wamepata ajira za moja kwa moja kupitia vyama vya ushirika.

Amesema pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto ya baadhi ya viongozi, wanachama na wadau kutokuzingatia uadilifu, hivyo TCDC kwa kushirikiana na COASCO na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) inaendelea kutekeleza kampeni ya “Linda Ushirika, Chagua Uadilifu”.