Na Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
WAZIRI wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Omar , amesema kuwa mafanikio yanayoendelea kushuhudiwa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi yanapaswa kuimarishwa kwa ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za Serikali, sekta binafsi na wadau mbalimbali ili kuongeza uzalishaji, thamani ya mazao na kukuza uchumi wa Taifa.
Amesema hayo Agosti 2, 2026, jijini Dodoma wakati alipotembelea Viwanja vya Dk. John Samuel Malecela vilivyopo Nzuguni, kwa ajili ya kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa katika Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Kilimo (Nane Nane) 2026.
Aidha, amesema kuwa lengo la maonesho hayo limefanikiwa kwa kuonesha fursa zilizopo katika sekta ya kilimo pamoja na mafanikio yanayopatikana kupitia uzalishaji wa mazao, mifugo na uvuvi.
Pia, amebainisha kuwa ipo haja ya kuendelea kufanya kazi kwa pamoja badala ya kila sekta kufanya kazi kivyake, akisisitiza kuwa maendeleo ya kilimo yanahitaji ushirikiano unaojumuisha kilimo, mifugo, uvuvi, viwanda na sekta ya fedha ili kuongeza uzalishaji na uchakataji wa mazao.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwekeza katika utafiti wa kilimo na mifugo kwani maeneo hayo yana uwezo mkubwa wa kuleta mageuzi ya uzalishaji endapo yatapatiwa rasilimali za kutosha.
Amesema kuwa baadhi ya taasisi za utafiti zimeonesha uwezo mkubwa wa kubadili sekta ya mifugo kupitia teknolojia na tafiti mbalimbali, hivyo kuna umuhimu wa kuongeza uwekezaji katika maeneo hayo kwa kuwa yanaweza kujigharamia na kuleta manufaa makubwa kwa Taifa.
Aidha, amesema kuwa ameridhishwa na maendeleo ya ufugaji wa samaki, akieleza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza upatikanaji wa protini kwa wananchi wakati ambapo uzalishaji wa samaki kutoka kwenye bahari na maziwa unaendelea kupungua kutokana na sababu mbalimbali.
Pia amebainisha kuwa matumizi ya teknolojia kupitia kituo cha huduma kwa wakulima (Call Center) yameongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za ugani kwa kuwa wakulima wanaweza kupata ushauri wa kitaalamu kwa njia ya simu bila kujali walipo nchini.
Ameongeza kuwa mfumo wa ufuatiliaji wa maafisa ugani kwa kutumia teknolojia ya GPS umeongeza uwajibikaji na kurahisisha Serikali kufahamu kwa wakati halisi maeneo wanayofanyia kazi maafisa hao.
Aidha,amesema kuwa Serikali imeendelea kutumia mifumo ya kidijitali kufuatilia matumizi ya matrekta na zana nyingine za kilimo ili kuhakikisha zinatumika kwa ufanisi na kuwafikia wananchi waliokusudiwa.
Huku akibainisha Kuwa amefurahishwa na ubunifu wa wajasiriamali wanaoshiriki maonesho hayo, huku akisisitiza umuhimu wa taasisi za viwango na ubora kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa zinakidhi mahitaji ya soko kabla ya kuanza kuuzwa.
Aidha, amebainisha kuwa changamoto iliyopo si ubora wa bidhaa pekee, bali pia uzalishaji wa kiwango kinachokidhi mahitaji ya soko pamoja na kuzitangaza bidhaa za Tanzania ili ziweze kutambulika zaidi ndani na nje ya nchi.
Pia ameongeza kuwa kaulimbiu ya maonesho ya mwaka huu ya “Tambua Soko, Zalisha kwa Tija, Ongeza Thamani” inalenga kuhakikisha wazalishaji wanazalisha bidhaa zinazokidhi ubora na kiwango kinachohitajika na soko.
Amesema kuwa kuongeza tija katika uzalishaji ndiyo msingi wa mageuzi ya sekta ya kilimo, akitolea mfano matumizi ya malisho bora yanayoweza kuzalisha chakula kingi cha mifugo katika eneo dogo, hatua inayoongeza uzalishaji na matumizi bora ya ardhi.
Kwa upande mwingine, amesema kuwa utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unategemea kwa kiwango kikubwa mageuzi ya sekta ya kilimo, ikiwemo mazao, mifugo, uvuvi na misitu, ambayo ndiyo msingi wa kukuza viwanda, biashara na uchumi wa nchi.
Amesisitiza kuwa ushirikiano, uwekezaji katika utafiti, matumizi ya teknolojia na kuongeza tija ndiyo nguzo muhimu zitakazoiwezesha Tanzania kufikia malengo ya maendeleo ya kiuchumi na kuongeza kipato cha wananchi katika miaka ijayo.

