Na Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) imeeleza kuwa matumizi ya mifumo ya kidijitali katika vyama vya ushirika yameleta mapinduzi makubwa katika usimamizi wa shughuli za ushirika nchini, huku zaidi ya vyama 6,000 vikisajiliwa kwenye mfumo maalum wa kidijitali.
Meneja wa Mawasiliano wa e-GA, Subira Kaswaga, amesema kuwa mfumo huo umewezesha kuongeza uwazi katika biashara za mazao, kupunguza mianya ya upotevu wa mapato pamoja na kuwapa wakulima uwezo wa kufuatilia mwenendo wa mauzo ya mazao yao kwa wakati.
Akizungumza August 2 ,2026 kwenye Maonesho ya Nanenane yanayoendelea jijini Dodoma, Kaswaga amesema kuwa mfumo huo umetengenezwa kwa ushirikiano na Tume ya Maendeleo ya Vyama vya Ushirika kwa lengo la kurahisisha uendeshaji wa shughuli za ushirika kupitia teknolojia.
Amesema kuwa kupitia mfumo huo, mkulima anaweza kupata taarifa kuhusu mazao aliyowasilisha, bei iliyopatikana sokoni pamoja na kiasi cha fedha anachopaswa kulipwa, jambo ambalo limeongeza uwajibikaji na kuimarisha uaminifu kati ya wakulima na vyama vya ushirika.
Aidha, amebainisha kuwa e-GA imeendelea kushirikiana na Wizara ya Kilimo pamoja na taasisi mbalimbali kuandaa na kuboresha mifumo ya kidijitali inayosaidia ukusanyaji wa taarifa za wakulima, utoaji wa huduma na usimamizi wa shughuli mbalimbali za kilimo.
Pia ameongeza kuwa mamlaka hiyo imeshirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuanzisha mfumo wa Fertilizer Information System (FIS), ambao unasaidia serikali kufuatilia mnyororo wa upatikanaji wa mbolea kuanzia wazalishaji, waagizaji hadi wasambazaji.
Aidha, amebainisha Kuwa mfumo huo umeongeza uwezo wa serikali kufuatilia mwenendo wa soko la mbolea na kusaidia kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo hizo kwa bei inayozingatia maelekezo yaliyowekwa.
Amesema kuwa pamoja na mifumo hiyo, taasisi za serikali zimeendelea kutumia huduma za kidijitali kama barua pepe za serikali na mfumo wa e-Office, ambazo zimeboresha mawasiliano na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi.
“Malengo yetu ni kuhakikisha matumizi ya TEHAMA yanarahisisha utoaji wa huduma za serikali na kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi kupitia mifumo ya kidijitali,” amesema Kaswaga.
Amesisitiza kuwa e-GA itaendelea kushirikiana na wizara na taasisi mbalimbali kuhakikisha teknolojia inaendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuongeza ufanisi, uwazi na maendeleo endelevu nchini.
