Picha no 179 na 183 Mkurugenzi wa Veta Kanda ya Nyanda za Juu Suzan Magani kushoto,akimsikiliza Mwanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi Veta Songea fani ya umeme wa magri Meshack Ngongi,akieleza namna ya mfumo wa umeme wa magri unavyofanya kazi wakati wa mahali ya wahitimu wa mafunzo ya mradi wa Dumisha Amani 2026 uliofadhliwa na Shirika la Maendeleo ya Umoja wa Mataifa(UNDP) mbapo jumla ya vijana 60 wamehitimu mafunzo hayo.

Picha no 184 Mkurugenzi wa Veta Kanda za Nyanda za Juu Suzan Magani kulia akiangalia kifaa maluum kinachotumika kupima uwezo wa taa za magari baada ya kutembelea karakana ya matengenezo ya magari kwenye Chuo cha ufundi Stadi Veta Songea,kulia Mkuu wa Chuo cha Veta Songea Rahabu Mwakatundu na katikati Afisa Miradi wa UNDP Josephene Sepeku.

Picha no215 Mkurugenzi wa Veta Kanda ya Nyanda za Juu Suzan Magani,akiangalia nguo aina ya batiki zinazotengenezwa katika Chuo cha ufundi Stadi(Veta)Songea Mkoani Ruvuma wakati wa sherehe za mahafali ya Wahitimu wa mafunzo ya Mradi wa Dumisha Amani.

…………

Na Mwandishi Wetu, Songea

VIJANA 60 wavulana 34 na wasichana17, wamehitimu mafunzo ya fani mbalimbali katika Chuo cha Ufundi Stadi Veta kilichopo wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma chini ya mradi wa Dumisha Amani uliofadhiliwa na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa(UNDP).

Mkurugenzi wa Veta Kanda ya Nyanda za juu Kusini Suzan Magan,amewataka wahitimu hao waendelee kujifunza,kuboresha ujuzi ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia Duniani na hayo yawe mwanzo wa mafanikio zaidi katika maisha yao.

Magani, amelishukuru Shirika la Mpango wa maendeleo ya Umoja wa Mataifa(UNDP) kufadhili mradi huo kwani limeonyesha namna taasisi za maendeleo zinavyoweza kushirikiana na Serikali kuwawezesha vijana kupata stadi za kazi na kujenga misingi ya amani na mashikamano wa Kitaifa.

“Nawaomba washirika wa maendeleo na wadau tuendelee kushirikiana na veta kuanzisha na kuendeleza miradi kama huu ili kuwafikia vijana wengi zaidi kwani mahitaji ya ujuzi wa kazi nchini yanaendelea kuongezeka,hivyo ni muhimu kuwekeza zaidi katika elimu na mafunzo ya ufundi stadi”alisema Magani.

Mkuu wa Chuo cha Veta Songea Rahabu Mwakatundu alisema,mafunzo ya mradi wa Dumisha Amani yamefanyika kwa muda wa wiki mbili na washiriki wamepata mafunzo ya nadharia na vitendo yaliyolenga kuwaongezea umahiri katika fani zao ili kuwawezesha kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira na kujiajiri.

Alisema, lengo la mradi huo halikuwa kuwapatia vijana ujuzi wa kiufundi pekee,bali kuwajengea uwezo katika maadili,uzalendo,utamaduni wa amani,mshikamamo wa kitaifa pamoja na stadi za maisha.

Aidha alisema, mafunzo yamelenga kuwaandaa wahitimu(vijana) kuwa wataalamu wenye weledi,waadilifu na raia wema watakaotoa mchango chanya katika maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Mwakatundu alisema,wahitimu wamejifunza ufungaji wa mifumo ya umeme,ufundi wa magari,ubunifu wa mavazi,teknolojia ya nguo,ufundi bomba pamoja na kuwaongezea maarifa,ujuzi na maadili ili wawe mabalozi wa amani na mendeleo katika maeneo ya kazi na jamii wanayoishi.

“Pia wamefundishwa kufunga mfumo wa kamera za ulinzi(CCTV)unaotumia nishati ya jua unaoweza kufanya kazi kwa saa 24 bila kutegemea umeme wa Tanesco,kuunganisha mfumo wa CCTV na simu ya mkononi kwa ajili ya ufuatiliaji wa maeneo kwa njia ya mtandao”alisema.

Mwakatundu, ametaja fani nyingine walizofundishwa ni pamoja na kufunga mfumo wa umwagiliaji kwa shughuli za kilimo,kufunga gutter za uvunaji wa maji ya mvua,kufunga pampu za kusukuma maji,matengenezo ya injini za magari,kutengeneza batiki za mshumaa,batiki za kuchora na sabuni.

Naye Afisa miradi wa Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa Josephine Sepeku,amewataka wahitimu kuhakikisha wanakwenda kutumia ujuzi waliopa kujiajiri ili waweze kujikwamua kimaisha.

Awali katika risala yao iliyosomwa na Sophia Mtela wahitimu hao wamelishukuru Shirika la maendeleo la umoja wa Mataifa(UNDP)GPF na CPP kwa kufadhili mradi wa Dumisha Amani.

Mtela alisema, mradi huo umewajengea uwezo,kupata elimu ya amani,stadi za maisha,ujuzi wa ufundi na ujasiriamali utakaowawezesha kujitegemea na kuchangia maendeleo ya jamii yetu na Taifa kwa ujumla.

Alisema, kwa muda wa wiki mbili wamejifunza namna ya kudumisha amani katika jamii,mbinu za kutatua migogoro kwa njia ya amani na maridhiano,kuimarisha uhusiano baina yao na taasisi mbalimbali,kuongeza ujuzi wa kitaalumu katika fani walizosomea na kupata stadi za maisha.