Mwandishi Mkuu wa Sheria, Bw. Onorius Njole amefungua mafunzo maalum kwa Mawakili wa Serikali nchini, yanayohusu Sheria ya Fedha (Finance Act). Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 30 Julai, 2026 Jijini Dodoma, ambapo Mawakili wa Serikali kutoka taasisi mbalimbali nchini wameshiriki kwa wingi katika mafunzo hayo kwa njia ya mtandao. 

Mafunzo ya Sheria ya Fedha kwa Mawakili wa Serikali, yameratibiwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria, na kuendeshwa na Wakufunzi kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria na Wizara ya Fedha.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Mwandishi Mkuu wa Sheria, ameeleza kuwa Sheria ya Fedha ni mhimili mkuu wa utekelezaji wa Bajeti ya Serikali, hivyo Mawakili wa Serikali wana mchango mkubwa katika kuchambua, kuandika, na kuhakikisha vifungu vyake vinakidhi mahitaji ya kisheria na kiuchumi. 

*“Mafunzo haya yanalenga katika kuwapitisha Mawakili wa Serikali ili muweze kufahamu nafasi yenu katika mchakato mzima wa uandaaji na ukamilishaji wa sheria hiyo muhimu kwa uchumi wa nchi.”* Amesema Mwandishi Mkuu wa Sheria.

Mwandishi Mkuu wa Sheria amesema kuwa, mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wa kiufundi Mawakili hao kuhusu mabadiliko mbalimbali ya kodi na fedha yanayoingizwa kwenye Sheria ya Fedha kila mwaka, na kuongeza ufanisi wakati wa kuandika muswada wa sheria hiyo (drafting process).

Aidha, Bw. Njole amesema kuwa mafunzo hayo yatajikita katika kujadili kwa kina nafasi ya Mawakili wa Serikali katika mchakato wa utengenezwaji wa sheria ya fedha, pamoja na kufahamu mfumo wa kisheria katika utekelezaji wa bajeti kuu ya Serikali.

*“Kupitia mafunzo haya tutapata uelewa wa pamoja, wajibu wa Mawakili wa Serikali wakati wa Utungwaji wa sheria na wakati wa utekelezaji wa sheria hii ya fedha.”* Amesema Mwandishi Mkuu wa Sheria.

Vilevile, Mwandishi Mkuu wa Sheria amesema kuwa kupita mafunzo hayo, Washiriki watapata kujifunza kwa undani kuhusu faida na malengo ya marekebisho mbalimbali yanayofanyika katika Sheria ya Fedha, na kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao.

Awali, akimkaribisha Mwandishi Mkuu wa Sheria, Kaimu Mkurugenzi wa Majadiliano, Usimamizi wa Mikataba na Utatuzi wa Migogoro, Bw. Edson Mweyunge aliwataka Washiriki wa mafunzo hayo kushiriki kikamilifu katika mada mbalimbali zitakazotolewa na wakufunzi, ili ziweze kuwasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. 

Wakufunzi wa mafunzo hayo wametoa mada katika maeneo ya Uundaaji wa Sheria ya Fedha, Masuala muhimu katika Sheria ya Fedha ya Mwaka 2026, Wajibu wa Wakili wa Serikali katika Sheria ya Fedha, Utekelezaji wa Sheria ya Fedha, na Utekelezaji wa Bajeti ya Serikali kupitia sheria ndogo.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza chachu na ufanisi kwa Mawakili wa Serikali katika kutekeleza majukumu yao ya uandaaji wa sheria, kutoa ushauri wa kisheria kwa Taasisi za Umma, na kuhakikisha utawala wa sheria unaendelea kuimarika nchini.