Mwandishi Wetu, Dar es Salaam, Julai 29, 2026
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari (JAB) imeanza rasmi kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari nchini, yakilenga kuimarisha weledi, maadili na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari wa Bongo FM jijini Dar es Salaam, redio dada ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi ya JAB, Tido Mhando, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa JAB, Wakili Patrick Kipangula, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wa kuelewa na kutekeleza matakwa ya Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229, kwa kuzingatia weledi, maadili na uwajibikaji.
“Mafunzo haya ni utekelezaji wa Sheria ya Huduma za Habari. Leo tumeanza rasmi na waandishi wa habari wa Bongo FM, tutaendelea kwa vyombo vingine pia kwa sababu, kutakuwa na mafunzo ya muda mfupi na ya muda mrefu. Hivyo, mafunzo haya yawe fursa ya kujenga uwezo na kuweka msingi imara wa kukuza na kulinda taaluma ya uandishi wa habari kwa kuongeza maarifa na weledi,” amesema Wakili Kipangula.
Akiwasilisha mada kuhusu Sheria ya Huduma za Habari, historia na uanzishwaji wake, katika mafunzo hayo yaliyoanza leo tarehe 29 Julai, 2026 katika ukumbi wa Bodi, Wakili Kipangula amesema sheria hiyo imeweka msingi wa kuimarisha taaluma ya habari kwa kubainisha viwango vya weledi, maadili na uwajibikaji.
Amesisitiza kuwa JAB itaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria hiyo kwa kuzingatia haki, uwazi na kuheshimu uhuru wa vyombo vya habari, huku ikihakikisha taaluma ya habari inalinda maslahi ya umma..
Aidha, amewataka waandishi wa habari kuzingatia sheria na maadili katika kila hatua ya ukusanyaji, uchakataji na usambazaji wa habari ili kujiepusha na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na ukiukaji wa taaluma.
Amesema kuzingatia misingi hiyo kunajenga weledi, kunalinda heshima ya taaluma na kuimarisha imani ya jamii kwa vyombo vya habari.
Kwa upande wake, Dkt. Egbert Mkoko, akiwasilisha mada kuhusu Maadili ya Uandishi wa Habari, amesema maadili ni nguzo muhimu ya taaluma inayojengwa katika misingi ya ukweli, usahihi, haki, mizania, uwajibikaji na kutanguliza maslahi ya umma.
Amesisitiza kuwa mwandishi wa habari hapaswi kuongozwa na kasi ya kuwahi kuripoti habari, shinikizo la mitandao ya kijamii, umaarufu au maslahi binafsi, bali na ukweli na uwajibikaji.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, akiwemo Bi. Irene Kilango na Bw. Anord Philemon, wameishukuru JAB kwa kuandaa mafunzo hayo, wakisema yamewaongezea uelewa kuhusu Sheria ya Huduma za Habari, maadili ya taaluma na wajibu wa mwandishi wa habari katika kutekeleza majukumu yake kwa weledi.
“Mafunzo haya yametupatia maarifa muhimu yatakayotusaidia kutekeleza majukumu yetu kwa kuzingatia maadili, sheria na viwango vya taaluma ya uandishi wa habari. Tunaamini yatachangia kuboresha utendaji wetu na kuongeza uwajibikaji katika kuhabarisha umma,” wamesema washiriki hao.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mpango endelevu wa JAB wa kuwajengea uwezo waandishi wa habari nchini ili kuhakikisha wanazingatia Sheria ya Huduma za Habari, maadili, weledi na viwango vya taaluma katika utekelezaji wa majukumu yao, kwa lengo la kuimarisha ubora wa huduma za habari na kulinda maslahi ya umma.

