Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Said Mtanda, ametunukiwa tuzo na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za kisheria kwa wananchi pamoja na kuendeleza misingi ya utawala bora mkoani humo.
Tuzo hiyo ilikabidhiwa na Wakili wa Serikali Mkoa wa Mwanza, Bw. Kabyemela Lushagara, katika hafla iliyofanyika Julai 29, 2026, katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Akizungumza wakati wa kukabidhi tuzo hiyo, Bw. Lushagara amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imetoa tuzo hiyo ikiwa ni sehemu ya kutambua ushirikiano na mchango wa Serikali ya Mkoa wa Mwanza katika kuimarisha utawala wa sheria na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za kisheria.
Kwa upande wake, Mhe. Mtanda ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutambua juhudi zinazofanywa na Serikali ya Mkoa wa Mwanza katika kusimamia utawala wa sheria na utoaji wa haki kwa wananchi.
Amesema tuzo hiyo ni chachu ya kuendelea kuongeza juhudi katika kuimarisha utawala bora na kuahidi kuendeleza ushirikiano na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuhakikisha wananchi wa Mkoa wa Mwanza wanaendelea kupata huduma za kisheria kwa ufanisi na kwa wakati.

