Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya laiomba jamii kusaidia malezi na makuzi ya watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu ili waweze kupata mahitaji muhimu.
Hayo yamezungumzwa na Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Anthony Mkwawa Julai 28, 2026 alipowaongoza Maafisa, Wakaguzi, Askari wa vyeo mbalimbali na watumishi wa Zahanati ya Jeshi la Polisi kutembelea na kutoa msaada kwa watoto wa kituo cha “Nuru Orphans Center”
ACP Mkwawa amesema kuwa, Jeshi la Polisi kama sehemu ya jamii limekuwa na utaratibu wa kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa makundi mbalimbali ya kijamii ili kuwawezesha kujikimu na kupata kupata mahitaji muhimu.
Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi Mbeya, Mrakibu wa Polisi (SP) Limwata Mganga amesema kuwa ushirikiano uliopo kati ya Jeshi la Polisi na jamii umekuwa ukizaa matunda hasa katika kuzuia na kutanzua uhalifu katika jamii.
Kwa upande wake, mmoja wa watoto wa kituo hicho, Melania Nuru amelishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa msaada walioutoa huku akieleza ndoto zake za kwenda kuendelea na masomo ya elimu ya juu katika Chuo cha Kodi Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa kituo hicho, Jason Fihangavo amesema kuwa kwa sasa jamii imeelimika na kumekuwa na idadi kubwa ya watu wanaofika kituoni hapo kwa ajili ya kuwachukua watoto katika utaratibu na kwenda kuwalea ikiwa ni pamoja na kuwasomesha na kuwapatia mahitaji muhimu.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia vikosi na vitengo mbalimbali limekuwa na utaratibu wa kurejesha kwa jamii)Corporate Social Responsibility) kwa kutembelea na kutoa msaada kwa makundi mbalimbali ya kijamii kwa lengo la kuimarisha mahusiano mazuri na ushirikiano katika kazi ya kuzuia na kutanzua uhalifu.

