Na Mwandishi Wetu, Chalinze
Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara haitakumbwa na changamoto ya kukatika kwa umeme wakati wa utekelezaji wa hatua za mwisho za Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze, Morogoro hadi Dodoma, unaotarajiwa kukamilika Agosti 21, 2026. Mradi huo unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye urefu wa kilomita 345 na ni sehemu ya kuimarisha miundombinu ya taifa ya umeme
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Irene Gowele, ambaye amesema kazi za mwisho za kuvuta nyaya zitafanyika katika maeneo ya Mkambalani mkoani Morogoro na Kikombo mkoani Dodoma, hivyo kulazimu kuzimwa kwa baadhi ya njia za kusafirisha umeme ili kuhakikisha usalama wa mkandarasi.
Amesema zoezi hilo litafanyika kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza itaanza Julai 30 hadi Agosti 4, 2026 katika eneo la Mkambalani, Morogoro, huku awamu ya pili ikifanyika Agosti 11 hadi 17, 2026 katika eneo la Kikombo, Dodoma.
Kwa mujibu wa Gowele, mikoa ya kanda ya kati, kaskazini, ziwa, magharibi na kusini magharibi itaathirika kwa nyakati tofauti, huku huduma ya umeme ikikosekana kati ya saa 12:00 asubuhi hadi saa 11:00 jioni kulingana na ratiba zitakazotolewa na TANESCO.
Amesisitiza kuwa hakutakuwa na kukatika kwa umeme kwa siku zote katika maeneo yote, bali kila eneo litaathirika kwa muda na siku tofauti. Ratiba za maeneo husika zitatangazwa kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na makundi rasmi ya WhatsApp ya TANESCO nchi nzima.
Akizungumzia manufaa ya mradi huo, Meneja wa Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Chalinze kwenda Dodoma, Mhandisi Newton Mwakifwamba, amesema mradi huo wenye thamani ya takribani shilingi bilioni 514 umefikia asilimia 94 ya utekelezaji.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha umeme wote unaozalishwa katika Bwawa la Julius Nyerere wenye uwezo wa megawati 2,115 kusafirishwa kwa ufanisi zaidi hadi kwa watumiaji, kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini na kuongeza uwezo wa Tanzania kushiriki biashara ya umeme ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Ukanda wa Kusini mwa Afrika.

