Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Elias Magosi, akizungumza wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Tisa ya Viwanda ya SADC (SADC Industrialisation Week 2026), inayoadhimishwa katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (ICC), jijini Durban, Afrika Kusini. Mkutano huo unawakutanisha viongozi wa serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo kujadili mikakati ya kuharakisha maendeleo ya viwanda na biashara ya kikanda.

Washiriki wa Wiki ya Tisa ya Viwanda kutoka nchi wanachama wa SADC wakifuatilia hotuba ya Mgeni Rasmi, Katibu Mtendaji wa SADC, Elias Magosi, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (ICC), Durban, Afrika Kusini.

Meneja wa Mawasiliano, Masoko na Mahusiano wa Benki ya Maendeleo – TIB, Bw. Allan Chonjo akitoa maelezo kuhusu bidhaa na huduma zinazotolewa na Benki hiyo kwa baadhi ya wadau waliotembelea Banda la Tanzania, pembezoni mwa Mkutano wa Wiki ya Viwanda ya SADC (SADC Industrialisation Week 2026) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (ICC), jijini Durban, Afrika Kusini.

Meneja wa Utafiti na Biashara kutoka Benki ya Maendeleo – TIB, Dkt.Hilderbrand Shayo akimkabidhi zawadi Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), Bi. Khadija Juma Ngasongwa alipotembelea Banda la Tanzania katika maonesho yanayofanyika sambamba na Wiki ya Tisa ya Viwanda ya SADC (SADC Industrialisation Week 2026) katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (ICC), Durban, Afrika Kusini.

Meneja wa Utafiti na Biashara Dkt.Hilderbrand Shayo na Meneja wa Mawasiliano, Masoko na Mahusiano Bw. Allan Chonjo, kutoka Benki ya Maendeleo – TIB wakitoa maelezo kuhusu bidhaa na huduma zinazotolewa na Benki hiyo kwa mdau aliyetembelea banda la Tanzania, pembezoni mwa Mkutano wa Wiki ya Viwanda ya SADC (SADC Industrialisation Week 2026) unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano (ICC), jijini Durban, Afrika Kusini. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Durban, Afrika Kusini)
…………..
Na Ramadhani Kissimba, Durban
Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) imezitaka nchi wanachama kuongeza kasi ya utekelezaji wa ajenda ya maendeleo ya viwanda kwa kuwekeza katika kuongeza thamani ya malighafi na kuimarisha miundombinu ili kukuza biashara, ajira na ustawi wa wananchi wa Jumuiya ya hiyo.
Wito huo umetolewa na Katibu Mtendaji wa SADC, Bw. Elias Magosi, wakati akifungua rasmi Wiki ya Tisa (9) ya Viwanda ya SADC (SADC Industrialisation Week 2026) inayofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Durban, Afrika Kusini.
Alisema kuwa ukanda wa SADC una rasilimali nyingi za kilimo, madini na nishati ambazo zinapaswa kutumika kama msingi wa kujenga uchumi wa viwanda badala ya kuendelea kuuza malighafi bila kuziongezea thamani.
Alisisitiza kuwa maendeleo ya viwanda hayawezi kufikiwa bila ushirikiano wa karibu kati ya serikali, sekta binafsi, taasisi za fedha na wadau wa maendeleo.
“Ushirikiano utasaidia kuvutia uwekezaji, kuongeza ushindani wa bidhaa za ukanda na kuimarisha biashara ndani ya SADC, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi jumuishi na wenye manufaa kwa wananchi wote” alisema Bw. Magosi.
Aidha, alizihimiza nchi wanachama kuwekeza katika miundombinu ya nishati, usafirishaji, TEHAMA na ubunifu, pamoja na kuwawezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na ujasiriamali wa viwanda.
Wiki ya Viwanda ya SADC imebeba kaulimbiu isemayo: “Kukuza Viwanda Imara, Endelevu na Jumuishi kupitia Maendeleo ya Miundombinu, Mageuzi ya Kilimo na Madini kwa Ajili ya Dunia Yenye Haki.” Ikihimiza matumizi ya rasilimali zilizopo katika nchi wanachama katika kujenga uchumi wenye ushindani, unaostahimili changamoto za kiuchumi na mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano huo wa siku tano unaowakutanisha Viongozi wa Serikali, sekta binafsi, wawekezaji, wataalamu na wadau wa maendeleo kutoka nchi wanachama wa SADC unatarajiwa kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha ushindani wa viwanda kwa nchi za SADC, kuvutia uwekezaji mpya na kuongeza thamani ya mazao ya kilimo pamoja na madini, ukiwa ni sehemu ya maandalizi kuelekea Mkutano wa 46 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC utakaofanyika tarehe 17 Agosti, 2026 Jijini Durban, Afrika ya Kusini.
