Kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia (WHC) ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kilichoanza tarehe 19 Julai, 2026 kinaendelea jijini Busan katika Jamhuri ya Watu wa Korea.

Mkutano huo unahudhuriwa na takriban watu 3,000, akiwemo Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO, wawakilishi kutoka Nchi Wanachama, maafisa wa ngazi ya mawaziri na naibu waziri kutoka nchi wanachama 21 wa Kamati ya Urithi wa Dunia, wajumbe kutoka nchi 196 zilizoridhia Mkataba wa Urithi wa Dunia, na vyombo vya ushauri vya UNESCO vya ICOMOS na IUCN.

Katika mkutano huo, Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika UNESCO umeandaa kikao cha pembeni kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA).

Tanzania imewasilisha mada na kuongoza majadiliano kuhusiana na zoezi la uhamaji wa hiari wa wananchi kutoka eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.

Bw.Thadei Aldo Kabonge, Katibu wa Tume ya Rais iliyofanya tathmini ya masuala ya ardhi katika Wilaya ya Ngorongoro aliueleza mkutano huo kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliteua Tume mbili kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wawakilishi wa jamii ya Wamasai kutoka Wilaya ya Ngorongoro wakati wa hadhira yao na mheshimiwa Rais iliyofanyika jijini Arusha mnamo Desemba 2024.

Tume ya kwanza ilipewa jukumu la kufanya tathmini na uchambuzi wa kina wa malalamiko hayo, ambayo yanatokana na migogoro ya matumizi ya ardhi na mipango ya uhifadhi wa serikali katika wilaya hiyo.

Bw. Kabonge aliueleza mkutano huo kuwa, Tume iliyoteuliwa na Mheshimiwa Rais ilikuwa na muundo mseto, na ilijumuisha watumishi watatu wa umma, watumishi wa umma watatu wastaafu, wawakilishi wawili kutoka jamii ya wafugaji wa Kimaasai kutoka Ngorongoro na Majaji wawili kutoka Mahakama ya Rufaa. Kufuatia tathmini ya kina ya miezi saba, Tume ilikusanya taarifa zenye takwimu muhimu thelathini na tatu. Hata hivyo, Bw. Kabonge alibainisha kuwa katika tukio la mkutano wa pembeni, anawakilisha matokeo sita ya msingi.

Kwa kuanzia, Kamati ilibaini ongezeko kubwa la idadi ya watu, lisiloendana na mahitaji yanayoongezeka ya maisha ya binadamu ambayo hayawezi kutoshelezwa na rasilimali za ndani za eneo la hifadhi ya Ngorongoro. Alibainisha kuwa, mnamo 1959, idadi ya watu wa NCA ilikuwa takribani 8,000 kulingana na taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu ya 2022, idadi ya watu imefikia laki moja na mia saba na tisini na tatu (100,793).

Kwa kasi hiyo, idadi ya watu inatarajiwa kuongezeka hadi mia mbili sabini na sita elfu, mia sita na hamsini na moja (276,651) ifikapo mwaka wa 2050 kwa kiwango cha wastani cha ukuaji wa 3.6% kwa mwaka.

Ongezeko hili la idadi ya watu limeendelea kusababisha mahitaji makubwa ya matumizi ya ardhi hivyo kuchochea ushindani kati ya uhifadhi, utalii, na maendeleo ya jamii katika eneo la ardhi ambalo haliongezeki.

Bw. Kabonge aliueleza mkutano huo kuwa, kwa upande wa mifugo, kamati ilibaini ongezeko kubwa la mifugo yaani ng’ombe, mbuzi, kondoo na punda wameongezeka kutoka mifugo mia mbili sitini na moja elfu mia saba ishirini na tatu (261,723) mwaka wa 1960 hadi kufikia mia saba kumi na tano elfu mia nne sitini na sita (715,466) katika mwaka wa 2022.

Inakadiriwa kuwa idadi ya ng’ombe pekee ambao wanahitaji eneo kubwa la malisho kuliko mifugo mingine itaongezeka kutoka ng’ombe mia mbili sabini na nne elfu mia tisa arobaini na tatu (274,943) mwaka wa 2022 hadi ng’ombe mia nne na kumi na nane elfu mia tisa na kumi na tatu (418,913) ifikapo mwaka wa 2050, wakihitaji eneo la kilomita za mraba 8,464.56, ambalo ni sawa na asilimia mia moja na nne (104%) ya eneo lote.

Bw. Kabonge alibainisha pia kuna ongezeko na mtawanyiko mkubwa wa makazi kwa sasa, ambapo makazi yameongezeka kutoka elfu kumi na tatu mia tatu na themanini na moja (13,381) mwaka wa 2019 hadi kufikia elfu kumi na saba mia saba thelathini na nne (17,734) mwaka wa 2025, sawa na ongezeko la asilimia 28.8.

Jinsi ongezeko na mtawanyiko wa makazi linavyoendelea kukua, maeneo ya malisho na shoroba za wanyamapori zinazidi kupungua na kuzidi kuhafifisha uhifadhi.Tume pia katika tathmini yake iliangazia uwezo wa wafugaji katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kujihimili kiuchumi na kuhakikisha usalama wa chakula na ilibaini kwa sasa uwezo wa kutegemea mifugo pekee unaendelea kupungua kwa kasi.

Bw. Kabonge alibainisha kuwa, Kamati ilibaini kiwango cha chini cha kujitosheleza kwa kutegemea mifugo pekee (Tropical Livestock Unit ama TLU) inahitaji ng’ombe wanane (8), kila mmoja akiwa na uzito wa kilo 250 kwa mahitaji ya mtu mmoja. Mnamo mwaka 2022, TLU kwa kila mtu katika NCA ilikuwa imedondoka hadi kufikia 3.5, na inakadiriwa kushuka zaidi hadi 1.5 ifikapo 2050.

Hii ina maana kuwa, jamii ya wenyeji wanaoishi ndani ya NCA inahitaji kuwa na shughuli mbadala au usaidizi mkubwa wa serikali ili kujihimili kiuchumi na kuhakikisha usalama wa chakula.

Bw. Kabonge alifafanua katika mkutano huo kuwa, kamati imebaini kuwepo kwa migogoro inayoongezeka kati ya binadamu na wanyamapori, ambapo wastani wa watu saba (7) wanauawa na wanyamapori kila mwaka kuanzia 2015 hadi 2025, na hivyo kuleta jumla ya watu 77 waliouawa na wanyamapori; zaidi ya hayo, watu 274 walijeruhiwa na mifugo elfu moja mia nne na hamsini (1,450) iliuawa na wanyamapori.Kutokana na changamoto zilizobainishwa, Tume iliwasilisha mapendekezo makuu kwa ajili ya Serikali kuyatekeleza ili kulinda utu, uhifadhi na kuwaletea wananchi maendeleo.

Bw. Kabonge aliutaarifu mkutano huo kuwa, Tume imependekeza yafanyike marekebisho ya mfumo wa kisheria wa NCA ili uendane na hali halisi ya mazingira ya sasa, kuhakikisha usawa wa kimkakati kati ya kipato cha jamii, maendeleo ya wananchi na uendelevu wa uhifadhi.Vile vile, Tume imeelekeza yatambuliwe maeneo mbadala kwa ajili ya wananchi kuhamia kwa hiari ambayo yana sifa zinazofanana na NCA, kwa wakazi ambao watapenda kuhamia katika maeneo hayo baada ya kupokea vifurushi vya kuvutia vya fidia ambavyo vimeandaliwa na serikali.

Tume ilishauri wakati wa kipindi cha mpito wakati Serikali inapoendelea kuweka mipango ya utekelezaji wa kimkakati wa maendeleo ya wakazi, wananchi wataendelea kuishi katika eneo hilo na kuendesha maisha yao na vile vile wanaotaka kuhama kwa hiari wataendelea kuhama.Tume pia imeelekeza uandaliwe mkakati maalum wa elimu ya umma unaolenga kuielimisha jamii ya Wamaasai, wadau na wakazi wengine na kuwashirikisha kikamilifu katika kila hatua ya kutekeleza mapendekezo ya Tume.6. Mfumo wa kisheria wa NCA wa 1959 uliopitwa na wakati.

Kwa kuzingatia vipindi ambavyo sheria hii imepitia na kuangalia mabadiliko makubwa ya sera, uhifadhi, kiteknolojia, na mazingira ambayo yametokea tangu wakati huo, ni wazi kwamba Sheria hii imepitwa na wakati na haionyeshi mahitaji ya sasa na hali halisi ya uhifadhi.