Na Happy Lazaro, Arusha
Waziri wa Kilimo na Mlezi wa Kiserikali wa Mkoa wa Arusha Mhe. Daniel Godfrey Chongolo amesema kazi kubwa inayoendelea kufanyika katika mradi wa ujenzi wa Uwanja wa michezo Jijini Arusha unaotarajiwa kutumika kwenye Michuano ya Soka ya AFCON 2027 ni dhihirisho la utayari wa Mkoa wa Arusha na Tanzania katika kuhodhi uenyeji wa michuano hiyo mikubwa zaidi kwa Ngazi ya Timu za Taifa za wanaume Barani Afrika.
Chongolo amebainisha hayo leo wakati wa ziara yake ya Kikazi kwenye wilaya ya Arusha, huku akimshukuru  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utayari wake wa kuridhia kuwa Mwenyeji wa mashindano hayo ya AFCON kwa kushirikiana na Mataifa ya Kenya na Uganda sambamba na kuridhia kutoa fedha za maandalizi ya michuano hiyo.
“Bila kuwa na haya mashindano ya AFCON 2027 tusingekuwa na huu uwanja leo, bila dhamira na utayari wa Rais na serikali hii tusingekuwa na maandalizi haya lakini uwanja huu pia unaenda kubadilisha sura ya eneo hili, wote mmeona barabara zinavyojengwa na namna ambavyo Vijana wengi wamepata ajira kwenye mradi huu na hii ndio namna serikali inayojua dhamana na wajibu wake kwa Nchi yake inavyofanya.”amesema  Chongolo.
Aidha Chongolo amepongeza uamuzi wa Serikali kujenga uwanja huo nje ya Jiji, akisema katika utekelezaji wake, fursa za uwekezaji zitafunguka zaidi hasa pia kutokana na kuwepo kwa ujenzi wa Kituo kikuu cha Mabasi Jiji la Arusha ambacho nacho kinajengwa kwenye Kata ya Olmoti.
Aidha pia, Chongolo ametoa wito kwa wananchi wa Arusha kuchangamkia fursa za kiuchumi zitakazotokana na ujio wa michuano ya AFCON 2027 pamoja na ujenzi wa Kituo cha Mabasi Jiji la Arusha, akisema mwingiliano wa watu utakaokuwepo utasababisha kuimarika na kukua kwa mzunguko wa fedha kwa wananchi wa Mkoa wa Arusha.
Aidha Chongolo akizindua nyumba za walimu katika.shule ya sekondari Kalimaji amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii huku wakijikita zaidi kwenye masomo ya sayansi ili waweze kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yaliyopo sasa hivi.
Akizungumza kwenye mradi wa stendi mpya ya Bondeni.City Chongolo amemshukuru Rais Samia kwa miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa mkoani.Arusha.
“Kwa kweli nimeridhishwa na miradi hii inayoendelea kutekelezwa katika mkoa wa Arusha kwani ipo ndani ya wakati na kukamilika kwa miradi hii itafanya Arusha uwe mkoa wa mfano kwa kuwa na miradi mikubwa ya maendeleo .”amesema Chongolo.
Akitoa maelezo kwenye mradi wa Bondeni.city ,Mhandisi Mshauri wa mradi huo Injinia Frank Abia amesema hadi sasa hivi mradi umefikia asilimia 69.62 na unatarajiwa kukamilika 30/11/2026 na unatekelezwa na kampuni ya Mohammed Builders Limited .
Aidha Waziri Chongolo katika ziara yake jijini Arusha amekagua ujenzi wa soko la Kilombero,kituo cha mabasi Bondeni City,kuweka jiwe la msingi katika ukumbi wa kisasa wa mikutano wa jiji,pamoja na kuzindua nyumba ya walimu katika shule ya sekondari Kalimaji iliyopo halmashauri ya jiji la Arusha.