Na Andrea Kadege, WAF-Arusha

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha elimu ya kinga kwa wananchi, akieleza kuwa ni silaha muhimu katika kuzuia magonjwa mengi na kupunguza gharama za matibabu nchini.

Dkt. Magembe ameyasema hayo leo Julai 25, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Arusha, Mount Meru, alipokagua utoaji wa huduma za afya na kuzungumza na Madaktari Bingwa na Bobezi wanaoshiriki kambi ya huduma za kibingwa ya upasuaji inayoendelea hospitalini hapo.

Amesema, magonjwa mengi yanayowafikisha wananchi hospitalini ni magonjwa yasiyo ya kuambukiza kama moyo, figo na mfumo wa upumuaji, yanaweza kuzuilika endapo wananchi watapata elimu sahihi kuhusu kinga na kuzingatia mtindo bora wa maisha, ikiwemo lishe bora, kufanya mazoezi na kuepuka vihatarishi vya afya.

“Serikali kupitia Wizara ya Afya itaendelea kutumia njia mbalimbali za mawasiliano kuwafikia wananchi, ikiwemo call center kwa namba 199, mitandao ya kijamii, redio, televisheni, magazeti pamoja na huduma za mkoba (outreach), ili kuhakikisha elimu ya afya inawafikia wananchi wengi zaidi” amesema Dkt. Magembe

Pia amewataka wataalamu wa afya kutumia kila fursa inayopatikana kutoa elimu, ikiwemo kwa wagonjwa na ndugu wanaosubiri huduma hospitalini kupitia televisheni na mifumo mingine ya mawasiliano, ili muda wa kusubiri huduma uwe sehemu ya kujifunza namna ya kujikinga na magonjwa.

Dkt Magembe ametumia jukwaa hilo pia kuwashukuru wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo ECSA HC, KIDS OR, na We Care Solar kwa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuratibu kambi za matibabu ya kibingwa ambazo zimesaidia kusogeza huduma karibu na wananchi na kupunguza gharama za kufuata matibabu katika umbali mrefu.