NA DENIS MLOWE, IRINGA

KATIBU wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Mkoa wa Iringa, Joseph Ryata, amewapongeza viongozi mbalimbali wa kitaifa kwa mchango wao katika ujenzi wa Kanisa la Lutheran Mlandege akisema ushirikiano wao unaonyesha namna Watanzania wanavyoweza kushirikiana bila kujali tofauti za dini.

Ryata alitoa kauli hiyo alipokuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mjumbe Kamati ya Siasa Mkoa wa Iringa Dickson Mwipopo katika ibada kuchangisha yenye lengo la ikununua basi aina ya Costa kwa ajili ya kwaya ya usharika ya kanisa la Lutherani Mlandege na kufanyika Kanisani hapo ambapo alisema viongozi hao walitoa mchango mkubwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba ya ibada kwa kutambua umuhimu wa kumtumikia Mungu na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.

Katika zoezi hilo la uchangiaji Jumla sh. million 19,5,40,000 zilipatikana ikiwa ni ahadi pamoja na fedha taslimu ambapo wadau mbalimbali walijitokeza kuchangia kanisa hilo ambapo 

mjumbe wa kamati ya siasa ya Ccm Mkoa wa Iringa Dickson Mwipopo alichangia milioni 5.

Ryata Alimtaja Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete kuwa alichangia ununuzi wa mabati yaliyotumika kuezeka kanisa hilo, huku akimpongeza pia Waziri Mkuu Lameck Mwigulu Nchemba kwa kuendelea kushiriki na kuhamasisha maendeleo ya kanisa hilo, licha ya majukumu yake makubwa ya kitaifa.

“Viongozi hawa hawakuangalia tofauti za dini walizotoka, bali waliangalia umuhimu wa kujenga nyumba ya Mwenyezi Mungu ambayo itatumika na waumini kumwabudu na kumtukuza Mungu,” alisema Ryata.

Alisema ushirikiano huo unapaswa kuwa mfano kwa Watanzania wote, kwani umoja na mshikamano ndiyo msingi wa kudumisha amani, utulivu na maendeleo nchini.

Ryata aliwataka wananchi kuendelea kuenzi utamaduni wa kushirikiana katika shughuli za maendeleo bila kujali tofauti za kidini au kimadhehebu, akieleza kuwa maendeleo ya jamii yanapatikana pale wananchi wanapoweka mbele maslahi ya taifa.

Aidha, alisema makanisa mbalimbali na waumini kutoka madhehebu tofauti wamekuwa wakishirikiana katika shughuli za maendeleo na kueneza Injili, jambo ambalo linaimarisha upendo na kuifanya Iringa kuendelea kuwa mfano wa mshikamano wa kijamii.

Alisisitiza kuwa viongozi wa dini na wananchi wana wajibu wa kuendelea kulinda umoja uliopo, ili kizazi cha sasa na kijacho kiendelee kuishi katika mazingira ya amani, kuheshimiana na kushirikiana kwa manufaa ya taifa.