MOSHI.

WANAWAKE wa rika zote, wakiwemo wafanyakazi na wasio na ajira, wamehimizwa kujitokeza kushiriki katika mkutano maalumu wa mafunzo ya biashara na maendeleo binafsi unaolenga kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.

Mwenyekiti wa mkutano huo, Agripina Boisafi, amesema lengo la kikao hicho ni kuwapa wanawake maarifa kuhusu fursa mbalimbali za biashara, mbinu za kujiajiri, pamoja na njia za kujiendeleza ili kuboresha maisha yao na ya familia zao.

Ameeleza kuwa kupitia mkutano huo, washiriki watapata elimu kuhusu uanzishaji na uendeshaji wa biashara, maendeleo binafsi, pamoja na fursa za kujiongezea kipato.

Boisafi amesisitiza kuwa mwaliko huo uko wazi kwa wanawake wote bila kujali umri, kiwango cha elimu au hali ya ajira, akibainisha kuwa kila mwanamke ana nafasi ya kujifunza na kunufaika na maarifa yatakayotolewa.

Mkutano huo unatarajiwa kufanyika Jumapili, Julai 26, 2026, kuanzia saa 7:00 mchana, katika ukumbi wa Kilimanjaro Crane, uliopo mkabala na Viva Supermarket.

Ametoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi ili kutumia fursa hiyo ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kujenga msingi wa maendeleo ya kiuchumi kwao na familia zao.