Na Atley Kuni, WAF-Kigoma
Wananchi zaidi 24,000 wa Manispaa ya Kigoma mjini wameendelea kupata elimu kuhusu ugonjwa wa Ebola kupitia kampeni maalumu ya uhamasishaji inayofanyika kwa kutumia gari la maalum la matangazo linalozunguka katika Manispaa hiyo na kutoa elimu ya afya pamoja na kugawa mabango na vipeperushi vyenye maelezo muhimu kwa ajili ya kujisomea na kusambaza ujumbe wa kujikinga na ugonjwa Ebola
Kampeni hiyo inayofanywa na Serikali kwa Ushirikiano na Mdau CIHEB Tanzania chini ya mradi wa Usalama wa Afya Duniani imefanyika Julai 22, 2026 na kutembelea masoko ya Buzebazeba, Kagera, Mwandiga, Gungu, Marungu na Kigoma Mjini, ambapo wananchi zaidi ya 24000 wamefikiwa wakati wa zoezi hilo.
Kupitia matangazo hayo, wananchi wamekumbushwa kuwa Ebola ni ugonjwa hatari wa kuambukiza unaosababishwa na virusi vya Ebola. Ugonjwa huu unaweza kuenea kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya kugusana na majimaji ya mwili wa mtu mwenye maambukizi, ikiwemo damu, mate, jasho, matapishi na majimaji mengine ya mwili. Pia maambukizi yanaweza kutokea kwa kugusa wanyama walioambukizwa bila kuchukua tahadhari.
Jamii imehimizwa kuendelea kuzingatia hatua za kujikinga na Ebola, ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi tiririka na sabuni, kutumia vitakasa mikono pale inapohitajika, kuepuka kugusana moja kwa moja na mtu mwenye dalili za ugonjwa bila kinga pamoja na kutoa taarifa mapema kwa mamlaka za afya endapo kutakuwa na mtu mwenye dalili zinazoweza kuashiria maambukizi.
Wananchi pia walielimishwa kuhusu dalili za Ebola ambazo zinaweza kujumuisha homa kali, uchovu, maumivu ya misuli na kichwa, koo kuuma, kutapika, kuharisha, upele na wakati mwingine kutokwa damu. Walisisitizwa kutafuta huduma za afya mapema pindi wanapoona dalili hizo ili kupata uchunguzi na msaada wa kitabibu kwa wakati.
Kampeni hiyo imelenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu ugonjwa wa Ebola, kuimarisha utayari wa jamii katika kuzuia maambukizi na kuhakikisha taarifa sahihi za afya zinafika kwa watu wengi zaidi.
Wananchi wameaswa kuendelea kutumia vipeperushi walivyokabidhiwa kama chanzo cha elimu na kuwafikishia wengine ujumbe wa kujikinga na Ebola ili kujenga jamii yenye uelewa na usalama zaidi dhidi ya magonjwa ya kuambukiza.

