Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Mwakilishi mpya wa UN Women nchini Tanzania, Bi. Julia Broussard, aliyefika Ikulu Zanzibar kujitambulisha rasmi, leo tarehe 22 Julai 2026. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Mwakilishi mpya wa UN Women nchini Tanzania, Bi. Julia Broussard, aliyefika Ikulu Zanzibar kujitambulisha rasmi, leo tarehe 22 Julai 2026.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akiwa katika picha ya pamoja na Mwakilishi mpya wa UN Women nchini Tanzania, Bi. Julia Broussard, baada ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Zanzibar kufuatia ziara yake ya kujitambulisha rasmi, Leo tarehe 22 Julai 2026

…………. 

Na Mwandishi Wetu
Zanzibar, Julai 22, 2026
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali iko tayari kushirikiana na UN Women kuboresha kilimo cha mwani kwa kuongeza uzalishaji, usarifu na thamani ya zao hilo ili kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Ikulu Zanzibar alipokutana na Mwakilishi mpya wa UN Women nchini Tanzania, Bi. Julia Broussard, aliyefika kujitambulisha baada ya kuanza rasmi majukumu yake. Amesema wanawake ndio nguvu kubwa katika sekta ya mwani, hivyo kuimarisha kilimo hicho kutawaongezea kipato, kufungua fursa zaidi za ajira na kupanua masoko ya zao hilo.

Aidha, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na UN Women katika kukuza usawa wa kijinsia, kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuimarisha juhudi za kuzuia na kutokomeza vitendo vya ukatili na udhalilishaji dhidi ya wanawake na wasichana.

Rais Dkt. Mwinyi pia amesisitiza umuhimu wa matumizi ya takwimu sahihi za kijinsia katika kupanga sera, programu na bajeti zinazolenga kukidhi mahitaji ya wanawake, akibainisha kuwa Serikali inaendelea kutoa nafasi zaidi kwa wanawake kushiriki katika uongozi na maamuzi.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa UN Women nchini Tanzania, Bi. Julia Broussard, ameahidi kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha kilimo cha mwani, kuwawezesha wanawake kiuchumi, kupambana na ukatili wa kijinsia na kutekeleza programu zinazochochea maendeleo jumuishi ya wanawake na wasichana.