Maandamano ya Julai 7 yaliyokuwa yamehamasishwa kwa nguvu kupitia mitandao ya kijamii yalitarajiwa kuvuta idadi kubwa ya wananchi kushiriki. Hata hivyo, hali iliyojitokeza siku hiyo ilikuwa tofauti na matarajio ya waandaaji, huku wananchi wengi wakiamua kubaki majumbani na wengine kufunga biashara zao kutokana na tahadhari ya kiusalama.

Wachambuzi wa masuala ya kijamii wanaeleza kuwa moja ya sababu zilizochangia maandamano hayo kutopata mwitikio mkubwa ni pengo lililopo kati ya wanaharakati wanaoishi nje ya nchi na hali halisi ya maisha ya wananchi waliopo Tanzania.

Kwa miaka kadhaa, wanaharakati wengi wa Kitanzania wamekuwa wakiishi nje ya nchi kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo changamoto za kisiasa, masuala ya usalama pamoja na kutafuta fursa bora za maisha.

Mfano unaotajwa mara nyingi ni wa Tundu Lissu ambaye aliondoka nchini baada ya kushambuliwa kwa risasi wakati wa utawala wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Baadaye alirejea nchini wakati wa uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuendelea na shughuli zake za kisiasa, ikiwemo kampeni ya No Reforms, No Elections. Hata hivyo, familia yake iliendelea kuishi nchini Ubelgiji ambako ilikuwa imepata hifadhi.

Kwa mujibu wa wachambuzi, hali ya viongozi wa harakati kuishi nje ya nchi hujenga changamoto ya kutokushiriki moja kwa moja mazingira wanayowataka wananchi wayakabili. Wakati wito wa maandamano unatolewa, viongozi hao pamoja na familia zao hubaki salama nje ya nchi huku wananchi waliopo Tanzania wakibeba athari zote zinazoweza kujitokeza.

Baada ya maandamano ya Julai 7, baadhi ya wanaharakati walioko nje ya nchi akiwemo Mange Kimambi na Maria Sarungi walieleza kuwa kufungwa kwa maduka na biashara kulikuwa ishara ya wananchi kuunga mkono maandamano hayo.

Hata hivyo, wananchi wengi walieleza kuwa sababu kubwa ya kutofungua biashara ilikuwa ni hofu ya vurugu pamoja na kulinda mali zao. Wengine waliona ni bora kupoteza mapato ya siku moja kuliko kuhatarisha usalama wao na biashara zao.

Aidha, kwa Watanzania wengi wanaotegemea kipato cha kila siku, kutofanya kazi hata kwa siku moja huathiri moja kwa moja uwezo wao wa kujikimu. Hivyo, hali hiyo ilikuwa changamoto kubwa kwa wananchi wa kawaida.

Wakosoaji wa harakati zinazoongozwa kutoka nje ya nchi pia wanakumbusha kampeni ya DontVisitTanzania, wakieleza kuwa licha ya kulenga kuishinikiza Serikali, walioathirika zaidi walikuwa wafanyakazi wa sekta ya utalii.

Miongoni mwao walikuwa waongoza watalii, wafanyakazi wa hoteli, madereva wa teksi za viwanja vya ndege pamoja na wananchi wengine waliokuwa wakitegemea mapato yatokanayo na utalii. Kwa mtazamo huo, baadhi ya wananchi wanaamini kuwa gharama za kampeni nyingi hubebwa na wananchi wa kawaida badala ya viongozi wanaolengwa.

Katika nchi nyingi zinazotoa hifadhi ya kisiasa, wahusika hupata msaada wa huduma mbalimbali ikiwemo makazi, elimu kwa watoto pamoja na huduma nyingine za kijamii.

Wachambuzi wanaeleza kuwa mazingira hayo yanaweza kuwafanya baadhi ya wanaharakati kushindwa kutambua kwa ukaribu changamoto zinazowakabili wananchi wanaoishi Tanzania kila siku. Hali hiyo pia imekuwa ikizua mjadala kuhusu uhalisia wa harakati zinazoongozwa kutoka nje ya nchi.

Aidha, ndani ya harakati hizo kumekuwa na mijadala kuhusu tofauti za kimtazamo kati ya wanaharakati wenyewe, huku baadhi wakituhumiwa kutumia lugha kali zaidi kuliko kujenga hoja zenye lengo la kuleta mabadiliko

Kwa ujumla, wachambuzi wanaona kuwa moja ya sababu zilizochangia maandamano ya Julai 7 kutofikia matarajio ni tofauti ya mazingira kati ya viongozi wa harakati wanaoishi ughaibuni na wananchi waliopo Tanzania. Wakati viongozi hao wanaendelea kutoa wito wa maandamano kupitia mitandao ya kijamii, wananchi waliopo nchini ndio wanaobeba athari za moja kwa moja za maamuzi hayo, ikiwemo kupoteza kipato, kuhatarisha usalama wao na kukabiliana na changamoto za maisha ya kila siku.