Na FARIDA MANGUBE MOROGOGO 

Mradi wa kuongeza uwezo wa kusimamia Sera za Uchumi Jumuishi (IGE) umechangia Tanzania kuimarisha ukuaji wa uchumi, uundaji wa ajira na usimamizi endelevu wa mazingira kwa kuunganisha watafiti na watunga sera katika kutatua changamoto za maendeleo.

Mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Sweden (Sida) unatekelezwa katika Nchini za Tanzania, Uganda, Kenya, Rwanda na Ethiopia kwa lengo la kuimarisha sera za uchumi jumuishi zinazochochea maendeleo bila kuathiri mazingira. 

Msimamizi Mkuu wa mradi huo nchini Tanzania kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Aloyce Hepelwa, amesema mradi umefanikiwa kuziba pengo lililokuwepo kati ya watafiti na watunga sera kwa kuwashirikisha katika kufanya tafiti na kuchambua changamoto zinazozuia ukuaji wa uchumi ili kupata suluhisho la pamoja.

Dkt. Hepelwa amesema kupitia Shule Kuu ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, mradi unasaidia matumizi endelevu ya rasilimali za asili ikiwemo maji, misitu, madini na kilimo ili kuongeza tija ya uchumi huku ukilinda mazingira. Ameeleza kuwa ushirikiano huo umewezesha tafiti kutumika moja kwa moja katika kuboresha sera na maamuzi ya Serikali yanayolenga maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Mtafiti Mwandamizi kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mhandisi Dkt. Befrina Igulu, amesema taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika kufanya tafiti zinazosaidia utekelezaji wa programu za uhifadhi wa mazingira na usimamizi wa rasilimali za asili kwa ufanisi zaidi.

Naye Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mazingira katika Wizara ya Kilimo, Dkt. Rose Mbezi, amesema licha ya changamoto zinazosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, sekta ya kilimo bado ni mhimili wa uchumi wa nchi nyingi za Afrika na pia imeendelea kutoa fursa mpya za maendeleo. Amesema takribani asilimia 70 ya Waafrika hutegemea kilimo kwa maisha yao, hivyo sera zinazochochea uchumi jumuishi na matumizi endelevu ya rasilimali ni muhimu katika kukuza uchumi na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.