Na Shaban Juma, WAF – Accra, Ghana

Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Florence Samizi amesema nchi za Afrika zinapaswa kuimarisha mshikamano, kuongeza uwekezaji katika sekta ya afya na kuharakisha utekelezaji wa sera zinazozingatia ushahidi wa kisayansi ili kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030, kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika vya akina mama na kuimarisha mifumo ya afya barani humo.Dkt. Samizi ameyasema hayo wakati akifungua Kikao cha 25 cha Dharura cha Baraza la Utendaji la Umoja wa Afrika, kinachofanyika jijini Accra, Ghana, ikiwa Tanzania ni Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Kiufundi ya Umoja wa Afrika ya Afya, Idadi ya Watu na Udhibiti wa Dawa (STC-HNPDC-5) akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe Mohamed Mchengerwa.

Amesema mkutano huo unafanyika katika kipindi muhimu ambapo nchi za Afrika zinaendelea kutekeleza Ajenda ya Afrika 2063 na Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), huku zikikabiliana na changamoto za magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza pamoja na changamoto nyingine mpya za afya zinazojitokeza katika bara hilo.

Aidha, Dkt. Samizi amesema licha ya Afrika kupiga hatua katika kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, bado bara hilo linakabiliwa na changamoto za vifo vya akina mama vinavyoweza kuzuilika, maambukizi ya VVU na kifua kikuu, magonjwa ya kitropiki yaliyosahaulika pamoja na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza yanayoendelea kuongeza mzigo kwa mifumo ya afya na uchumi wa nchi wanachama.

Dkt. Samizi amesema kikao hicho ni fursa muhimu ya kuthibitisha upya dhamira ya kisiasa ya nchi wanachama, kuimarisha ushirikiano na kuharakisha utekelezaji wa sera na uwekezaji endelevu utakaoboresha afya na ustawi wa wananchi wa Afrika, huku kikitoa nafasi ya kubadilishana uzoefu, ubunifu na mbinu bora za kukabiliana na changamoto za afya.

Ameongeza kuwa wajumbe wanatarajiwa kujadili masuala ya uzalishaji wa bidhaa za afya ndani ya Afrika, mifumo bunifu ya ufadhili wa sekta ya afya, uongozi wa kisiasa katika afya pamoja na kupitisha Azimio la Ngazi ya Juu kuhusu utekelezaji wa Ramani ya Umoja wa Afrika ya mwaka 2030 na kuendelea.

Akihitimisha hotuba yake, Dkt. Samizi amewataka wajumbe kushiriki kikamilifu katika majadiliano, kufanya kazi kwa mshikamano na kuibua suluhisho zenye tija zitakazowezesha Afrika kufikia lengo la Huduma za Afya kwa Wote (UHC) na kuhakikisha kila Mwafrika anapata huduma bora za afya na ustawi ifikapo mwaka 2030.