Na Hellen Mtereko,Geita

Waziri wa Madini Antony Mavunde, amewapongeza wawekezaji wazawa kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya madini, akisema hatua hiyo inaongeza thamani ya rasilimali za nchi, inachochea ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Aidha, ameonya kuwa Serikali haitasita kufuta leseni za uchimbaji kwa wamiliki wa maeneo ambao wameendelea kuyashikilia kwa muda mrefu bila kufanya shughuli za uzalishaji.Mavunde ameyasema hayo Julai 21,2026 wakati wa ziara yake katika kiwanda cha uchimbaji na uchakataji wa madini cha TAMPMED kilichopo Makurugusi, Wilayani Chato Mkoani Geita, kinachojengwa na wawekezaji wazawa wa Tanzania.

Amesema Serikali inathamini wawekezaji wanaowekeza kwa vitendo na kuongeza thamani ya madini badala ya kushikilia leseni bila kuendeleza maeneo ya uchimbaji.

“Wawekezaji wanaofanya kazi kama TAMPMED wanapaswa kupewa nafasi ya kuendelea kuwekeza hatuwezi kuendelea kuvumilia watu wanaoshikilia leseni kwa miaka mingi bila uzalishaji. Serikali itazifuta leseni hizo na kuwapa fursa wawekezaji wenye uwezo na dhamira ya kuendeleza sekta ya madini,” amesema Mavunde.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigela, amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini, hali ambayo imewezesha kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia za kisasa katika sekta ya madini. Amesema uwekezaji wa kampuni ya TAMPMED unaonyesha uwezo wa wawekezaji wazawa, huku zaidi ya shilingi bilioni nne zikiwekezwa katika ujenzi wa kiwanda hicho.

Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya TAMPMED, Ramadan Tampela, amesema ujenzi wa kiwanda hicho umegharimu zaidi ya shilingi bilioni nne na kitatoa huduma mbalimbali ikiwemo uchimbaji, uchenjuaji wa madini, uchomaji wa kaboni, upimaji wa sampuli zaidi ya 600 kwa maabara pamoja na huduma za kemikali, hatua itakayoongeza thamani ya madini yanayozalishwa nchini.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Makurugusi wamesema ujio wa kiwanda hicho umeleta matumaini mapya kwa jamii, wakieleza kuwa tayari vijana wengi wamepata ajira huku shughuli za kiuchumi zikiongezeka kutokana na uwekezaji huo.

Wamesema wanaamini kukamilika kwa kiwanda hicho kutachochea maendeleo zaidi ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.